Huwezi kusikiliza tena

Kisa na Mkasa na Salim Kikeke

Simu

Image caption Simu ya mkononi

Bwana mmoja nchini Marekani aliyenunua simu kupitia kwenye mtandao wa internet, amejikuta akinunua simu yake ambayo iliibiwa.

Bwana huyo mkazi wa California, alikuwa akirambaza kwenye mtandao, akitafuta simu nzuri na ya bei poa, na mara akavutiwa na simu ambayo aliona ina mvuto wa kipekee. Gazeti la Metro la London limesema bwana huyo akirambaza kwenye ukurasa wa craigslist.com alivutiwa na simu hiyo na kuinunua.

Image caption Mambo ya mtandao

Kwa mujibu wa ofisi ya liwali ya California, baada ya simu hiyo kuwasili kwa njia ya posta ndipo mteja huyo aligutuka. "Yaani namba zangu zoote zilikuwa bado zipo" amesema bwana huyo. Moja kwa moja alikwenda kutoa taarifa polisi. Baada ya polisi kuarifiwa, walikweda kumkamata kijana Neil Hefner mwenye umri wa miaka 28, ambaye ndio alikuwa muuzaji wa simu hiyo.

Polisi walikuta simu mia moja na sitini na tatu za wizi katika nyumba hiyo, huku kukiwa pia na pochi za watu, compyuta na vitu vingine vya thamani. Kosa alilofanya mwizi huyo ni kuweka anuani yake, wakati akituma simu aliyoiuza, ambayo ilisababisha kukamatwa kirahisi-- wamesema polisi.

Kunyweni na vuteni

Image caption Piga mtungi tu

Waziri wa fedha wa Urusi Alexei Kurdin amewataka wananchi wa hujo kunywa pombe kwa wingi na kuvuta sigara zaidi ili kusaidia kukuza uchumi wa nchi hiyo.

Ingawa mara nyingi wanasiasa huwataka wananchi kuzingatia afya bora, bwana Kurdin amewataka wananchi wake kupiga tungi na kuvuta sigara zaidi ili mapato ya taifa yaongezeke. "Ukivuta pakiti moja ya sigara, inamaanisha unasaidia kutatua matatizo ya kijamii" amesema waziri Kurdin. "Watu lazima waelewe, wale wanaokunywa na wavutaji, mnasaidia sana kujenga nchi" ameongeza waziri huyo.

Image caption Na fegi kwa wingi tu

Urusi, ambayo inafahamika kwa matumizi makubwa ya tumbaku na pombe, ni moja ya nchi yenye kodi ya chini kabisa ya bidhaa hizo katika nchi za Ulaya. Mwezi Juni mwaka huu mipango ya kuongeza mara dufu kodi ya sigara ilipangwa. Wizara ya fedha ya nchi hiyo bila shaka itarajie upinzani mzito kutoka kwa wananchi wa Urusi ambao wanapenda sigara. Si siku nyingi, upungufu wa sigara madukani ulizusha sokomoko nchini humo.

Msaka mizuka

Msaka mizuka na majini mmoja nchini Marekani amekufa baada ya kugongwa na treni, wakati akivizia kuona mzuka wa treni.

Image caption Ya mzuka huenda huonekana hivi

Christofer Kaiser mwenye umri wa miaka 29, alikuwa akitembea juu ya reli huko North Carolina alipokutwa na mkasa huo. Bwana Christofer akiwa na wasaka mizuka wenzake, walikuwa wakitembea juu ya mataruma ya reli Ijumaa iliyopita, wakivizia kuona mzuka wa treni iliyopata ajali katika eneo hilo miaka mia moja na kumi na tisa iliyopita.

Badala ya kuona mzuka, wasaka mizuka hao walitokewa na treni ya ukweli iliyokuwa na vichwa vitatu na behewa moja.

Image caption Hii ya ukweli

Wasaka mizuka wote walifanikiwa kuikwepa treni hiyo isipokuwa Christofer. Gazeti la Colombia Daily Tribune hata hivyo limesema bwana Christofer kabla ya kugongwa na terni hiyo alifanikiwa kumuokoa mwenzake mmoja kwa kumsukuma nje ya reli. Mwezi Agosti mwaka 1891, treni ya abiria iliacha reli na kusababisha vifo vya abiria thelathini. Kumekuwa na tetesi kuwa, kila mwaka katika tarehe ya ajali hiyo, sauti za abiria hao husikika katika eneo hilo, na mzuka wa treni huonekana.

Walalavi Nigeria

Image caption Usichelewe kuamka

Wafanyakazi wanaopenda kulala mno nchini Nigeria wamekomeshwa hivi karibuni baada ya kufungiwa nje ya ofisi zao, baada ya kufika makazini mwao wakiwa wamechelewa.

Mtandao wa chron.com umekaririwa ukisema -- katika harakati za kuleta mwamko kwa wazembe mjini Abuja, mamia ya wafanyakazi walifungiwa nje ya ofisi zao siku ya Jumanne wiki hii. Hatua hiyo ipo katika mpango unaoendelea wa serikali, wa kumaliza uchelewaji wa wafanyakazi makazini katika taifa hilo lenye watu wengi zaidi barani Afrika.

Image caption Hadi saa nne--

Taarifa zinasema milango hatimaye ilifunguliwa kwa wafanyakazi hao, saa moja baadaye na wachelewaji wakaruhusiwa kuingia. Hata hivyo, saa za kiafrika, bado zinalizonga taifa hilo lenye utajiri mkubwa wa mafuta na watu milioni mia moja na hamsini. Ofisi za serikali hutakiwa kuwa wazi saa mbili kamili asubuhi, lakini kutokana na ulalavi, ofisi hizo hufunguliwa saa mbili baadaye yaani saa nne. Ofisi hizo hutakiwa kufungwa saa kumi jioni kisheria -- lakini mara nyingi hufungwa mara tu umeme unapokatika-- jambo ambalo hutokea mara kwa mara.

BA yatisha abiria wake

Image caption Ndege ya BA

Shirika la ndege la Uingereza BA limeomba radhi abiria wake, baada ya kuwatangazia abiria hao, wakiwa angani kuwa ndoge wanayosafiria inataka kutua kwa dharura baharini.

Abiria wapatao mia mbili na sabini na watao waliokuwa katika ndege kutoka hapa London kuelekea Hong Kong siku ya Jumanne, walipatwa na mashaka na wasiwasi baada ya tangazo hilo kusikika katika spika ndani ya ndege hiyo. Ndege hiyo iliwa ikisafiri juu ya bahari ya kaskazini wakati huo. Shirika la habari la Reuters limesema, abiria walianza kusali sala zao za mwisho, wakijua huenda wasisalimike. "tulidhani ndio tunaenda kufa" amesema Michelle Lord, akizungumza na gazeti la the Sun. Abiria mwingine alisikika akisema hakuna jambo baya zaidi unalotarajia kusikia kama kutangaziwa kuwa ndege inataka kuanguka.

Image caption Ndege ya BA

Hata hivyo tangazo hilo lilitangazwa kimakosa. Wafanyakazi wa ndege hiyo, mara moja baada ya kugundua kosa hilo walianza kuwatuliza abiria hao, ambao wengine tayari walikuwa wamekaa mkao wa kutua kwa dharura. Msemaji wa shirika la ndege la Uingereza amesema uchunguzi unafanyika ili kujua kama lilikuwa kosa la kibinaadam, au ni la kompyuta.

Na kwa taarifa yako.....Mbuzi hawana meno ya juu ya mbele...

Tukutane wiki ijayo... Panapo Majaaliwa.....

Habari zimekusanywa kutoka vyanzo mbalimbali kwenye mtandao wa internet.