Huwezi kusikiliza tena

Kisa na Mkasa na Salim Kikeke

Mzee mgawa fedha

Polisi nchini Ujerumani waliitwa haraka katika mtaa moja kwenda kumkamata mtu aliyekuwa akigawa fedha kwa wapita njia.

Image caption Mzee alikuwa akigawa Euro moja kwa kila mpita njia

Kwa mujibu wa gazeti la Toronto Sun, wakazi wa Berlin walipatwa na mashaka na kuona labda ni mbinu ya uhalifu baada ya mzee kusimama kwenye mtaa uitwao Frohsinnstrasse, au mtaa wa uchangamfu, katika mji wa Aschaffenburg. Bwana huyo alikuwa amevaa bango kubwa mwili linalosema, " Sio kwamba sina kazi wala nyumba. Nina mke, na mambo yangu ni mazuri, na ndio maana nakupatia pesa". Mmoja wa wapita njia, akiona labda ni ujanja wa kuwaibia watu fedha, alipiga simu polisi haraka.

Image caption Pesa

Polisi walipigwa na butwaa walipofika kumhoji bwana huyo, aliyewaambia kuwa ni fedha zake za mafao ya kustaafu, na alikuwa akizigawa kwa kufurahia kustaafu.

Bwana huyo ambaye hakutajwa jina amesema, amefurahi kufikia umri wa kumaliza kufanya kazi, na alitaka furaha yake iwafikie na watu wengine. Baada ya kujieleza hivyo, bwana huyo mstaafu, aliruhusiwa kuendelea kugawa fedha zake, kwa sababu hakuna sheria inayosema mtu haruhusiwi kutoa fedha kwa wapita njia.

Jambazi juha

Mwizi mmoja wa benki, nchini Marekani, amekamatwa kirahisi kama kuku wa kisasa baada ya kushawishiwa na wafanyakazi wa benki, kukaa kitako na kufanyiwa mpango wa kupewa mkopo badala ya kufanya uhalifu.

Image caption Polisi wakaja kumkamata kirahisi kabisa...

Inadaiwa kuwa Mark Smith mwenye umri wa miaka hamsini na mitano, aliwaambia wafanyakazi wa benki mjini Watsonville, California, kuwa amebeba bomu katika begi lake, na kuwa atalilipua iwapo hatopewa fedha taslimu dola elfu mbili. Baada ya kuwatisha wafanyakazi hao, alitokea meneja wa benki hiyo na kumsihi jambazi huyo akae kwenye kiti ili wajadili matatizo yake ya kifedha. Baada ya mwizi huyo kukubali kukaa chini, meneja alianza kumuambia kuwa angeweza kumfanyia mpango wa kupata mkopo.

Image caption Jambazi juha

Wakati jambazi Smith akisubiri kwa hamu kuletewa fomu za kujaza apatiwe mkopo wake, meneja huyo wa benki alipata mwanya wa kupiga simu polisi. "kufikiri kwa haraka haraka kumeweza kusababisha mwizi kukamatwa kirahisi" amesema Ly Darren wa benki hiyo akizungumza na gazeti la Santa Cruz Sentinel. Polisi walimkamata mwizi huyo na kumshitaki kwa makosa ya kutaka kufanya wizi, na pia kutishia kulipua bomu, ambalo hata hivyo halikuwa la ukweli.

Juha zaidi...

Mwizi mwingine hapa Uingereza ametoa kituko cha mwaka, na kurahisisha kazi ya polisi, baada ya kudondosha simu yake ya mkononi katika nyumba aliyoenda kuiba.

Image caption 'Rudisha haraka simu yangu'

Gazeti la Metro la hapa London limesema baada ya mwizi huyo kuiba laptop katika nyumba moja mjini Cambridge, aligundua kuwa amepoteza simu yake. Akiwa hana uhakika simu yake iko wapi, mwizi huyo Anthony Gawthrop, alituma ujumbe mfupi wa maandishi, yaani text messege, yenye vitisho, ikisema " Kama wewe ndio una simu yangu rudisha haraka".

Image caption 'Kajileta mwenyewe' labda ndio polisi waliwaza

Kwa bahati mbaya, au nzuri, polisi ndio walikuwa na simu hiyo, waliyoikuta kwenye nyumba iliyofanyiwa wizi. Simu hiyo pia ilikuwa na picha kadhaa za mwizi huyo, na mara moja polisi waliweza kumgundua bwana huyo, kwani aliwahi kukamatwa kwa kufanya uhalifu katika siku za awali.

Mwanamama 'hayawani'

Mwanamke mmoja ametiwa nguvuni nchini Marekani, baada ya kuiba teksi aliyokuwa akitaka kuikodisha.

Image caption Taxi ya Marekani

Mwanamke huyo Jennifer Gille, mwenye umri wa miaka ishirini na tisa, aliingia katika teksi moja mjini Michigan, kama saa nane hivi ya usiku na kumuambia dereva ampeleke mji uitwao Covington, uliopo Louisiana. Dereva alikataa katakata, kwa sababu, Louisiana ni karibu maili elfu moja na mia mbili. Dereva huyo alipogoma, mwanamke huyo akiwa kaghadhibishwa, aliamua kuvua nguo zake zote kwa hasira.

Dereva wa taksi kuona hivyo, alimuamuru kutoka ndani ya gari, na mwanamama huyo alipogoma haraka aliwasha gari lake, na moja kwa moja akaelekea polisi. Kwa bahati mbaya alipofika polisi na kushuka kwenda kushitaki, alisahau kuchukua na funguo wa gari. Mwanamke huyo --abiria, mara aliruka katika kiti cha dereva, na huyoo kutokomea na taxi.

Hata hivyo kwa mujibu wa polisi wa huko, mwanamama huyo hakwenda mbali, kwani walimkuta mitaa michache tu kutoka kituo cha polisi, akiwa kaegesha gari na amelala fofofo, huku akiwa bado hana nguo. Msemaji wa polisi wa Michigan amesema, mwanamama huyo Jennifer ameshitakiwa kwa makosa ya kuvua nguo hadharani na wizi wa gari. Msemaji huyo ameongeza kuwa bibie huyo alikuwa amelewa, ingawa hakusema bayana kilikuwa ni kelvi gani.

Kiongozi wa maisha

Kwa wanasiasa wa kwetu bila shaka watavutiwa na habari hii. Waziri mkuu wa Urusi Vladimir Putin amesema yeye pamoja na waziri mkuu wa Italia, Sylvio Berlusconi, wanaweza kuendelea kukaa madarakani hadi watakapofika umri wa miaka mia moja na ishirini.

Image caption Putin na Berlusconi

Bwana Putin alikuwa akizungumza kufuatia ombi la bwana Berlusconi kutaka wakutane nchini Urusi ili kujadili jinsi ya kusaka fedha za kuongeza umri wa kawaida kuishi. Kwa mujibu wa BBC Bwana Berlusconi amesema inaweza ikawa kazi ngumu kubakia madarakani kwa muda mrefu huku ukiwa na majukumu mazito. Amesema hajawahi kuchukua mapumziko ya hata siku moja kwa mwaka mzima. Bwana Berlusconi alikuwa akikutana na bwana Putin kuhudhuria mkutano wa sera za ulimwengu mjini Moscow.

Bwana Berlusconi amesema taaisis hiyo inapanga kufadhili utafiti wa kuongeza umri wa binaadam kufikia miaka mia moja na ishirini, na huku akitabasamu akaongeza "nimeambiwa kuwa viongozi wataishi maisha marefu zaidi". Na hapo ndipo bwana Putin aliposema "kwa hiyo tutaendelea kuwa mawaziri wakuu mpaka tukifika miaka mia moja na ishirini". Berlusconi ana miaka sabini na nne, huku Putin akiwa na miaka hamsini na minane. Hata hivyo, wanasaisa wa kwetu msipate imani ya kufanya hivyo na ninyi, kwani waziri mkuu Putin na Berlusconi walikuwa wakifanya mzaha tu.

Na kwa taarifa yako....... Wanaume wanaweza kusoma maandishi madogo kuliko wanawake, lakini pia wanawake wana uwezo mkubwa zaidi wa kusikia kuliko wanaume.

Tukutane Wiki Ijayo Panapo Majaaliwa,,,,,

Habari zote kutoka vyanzo mbalimbali kwenye mtandao.