Huwezi kusikiliza tena

Kisa na Mkasa na Salim Kikeke

Harusi ya nyani

Image caption Bwana harusi

Baada ya kusikia ndoa ya mwa wiki iliyopita, wiki hii kumekuwa na harusi ya nyani katika hifadhi ya wanyama nchini Uchina. Bwana harusi alikuwa Yangyang mwenye umri wa miaka minne, ambaye amefunga ndoa ya bibi harusi Wanxing ambaye amemzidi kidogo umri mumewe, akiwa na miaka sita. Akiwa amejawa na aibu nyingi usoni, bwana harusi amefunga ndoa huku akiwa kazungukwa na wapiga picha.

Gazeti la metro limesema ingawa halina uhakika kama kweli nyani harusi hiyo alikuwa akiona aibu au la, na swali kuzuka-- je nyani wanaona aibu?.

Image caption Nyani anaona aibu

Hata hivyo taarifa kutoka huko zinasema ndoa yenyewe ilikuwa wa kuchaguliwa mchumba, kwani bwana harusi, Yongyang ni mzaliwa na Guinea barani Afrika, na alipelekwa katika hifadhi ya wanyama ya Hefei katika jimbo la mashariki la Anhui nchini Uchina.

Hatua hiyo ilifuatia waangalizi wa wanyama mwaka jana kuamua huyo ndio anafaa kumuoa Wanxing. Harusi yenyewe haikuwa kama hizi ambazo umezizoea, kwani bibi harusi alivaa kitop, au blauzi ya rangi ya pinki na kofia ya rangirangi, huku bwana harusi akiwa kavalia shati la rangi ya kijani, na bluu na sweta la manjano.

Fahali wazimu

Fahali moja nchini Uchina ambalo lilikuwa na hamu ya kutaka kupanda ngombe limeleta kizazaa na kuharibu magari.

Image caption Fahali lilipata ghadhabu

Fahali hilo lenye uzito wa tani moja na nusu lilikuwa limetoroka katika shamba moja mjini Nanning kusini mwa Uchina katika harakati za kutafuta ngombe jike, na likaingia mitaani kwa hasira na kuanza kufanya vurugu.

Baada ya kusaka ngombe jike bila mafanikio, dume hilo liliingia katika duka moja la magari na kuanza kuyavurumisha kwa kutumia mapembe yake. Polisi ambao walikuwa tayari kumpiga risasi na kumuua fahali huyo, walibembelezwa na wakazi wa mji, ambao walipiga simu kuwaita wataalam wa wanyama. Mtandao wa gazeti litolewalo bure hapa London la Metro limesmea wataalam wa wanyama hatimaye walipata wazo la kumtuliza fahali huyo kwa kumletea ngombe jike ambaye yuko katika katika msimu.

"Yaani alibadilika ghafla" amesema msemaji wa polisi. "dakika moja alikuwa na hasira akivunja magari, dakika nyingine alikuwa mpole kama kondoo" ameongeza polisi huyo.

Hii inaonesha jinsi mwanamke anavyoweza kumpoza mwanaume...

Amesema msemaji huyo wa polisi.

Kiboko wa Pink

Image caption Kiboko

Kiboko wa aina yake ameonekana kwa mara ya kwanza nchini Kenya. Kiboko huyo mwenye rangi ya pinki ameonekana akichezacheza katika dimbwi la maji na matope, huku rangi yake ikionekana wazi kuwa tofauti na familia yake.

Wapiga picha kutoka Uingereza Will na Matt walipiga picha za kiboko huyo katika mbuga ya wanyama ya masai mara wiki iliyopita. " Ni Kadogo kuliko viboko wengine na kila mara alikuwa pembeni ya mama yake" amesema will. "ilikuwa hali ya kupendeza kuona viboko wengine hawambagui, ingawa alikuwa na aibu sana, manake alivyotuona tu, akaingia kwenye maji na kujificha" amesema mpiga picha huyo.

Image caption Kiboko

Viboko wa rangi ya pinki huwa wana seli damu nyeupe. "mara nyingi wanyama hawa wenye maradhi ya ngozi wanashindwa kuishi porini kwa sababu wanaonekana kirahisi na pia huungua na jua haraka" amesema Will. Viboko wa aina hii hata hivyo wamewahi kuonekana nchini Uganda, lakini asilan nchini Kenya.

Mbwa apewa 'ridandasi'

Hali ya kifedha imekuwa mbaya mno katika jiji moja huko Pennsylvania nchini Marekani, hadi wamelazimika kumfukuza kazi mbwa wa polisi ili kubana matumizi.

Image caption Mbwa wa polisi

Baraza la jiji la Jeannette, Jumanne wiki hii lilipiga kura ya kupunguza kazi wafanyakazi tisa kati ya wafanyakazi 47 wa jiji ifikapo Oktoba tano. Polisi watatu wameachishwa kazi akiwemo Justin Scalzo na mbwa wake Wando, ambaye ni maarufu kwa kunusa na kukamata dawa za kulevya.

Mkuu wa polisi wa huko Brad Shepler amesema kuachisha kazi huko kumekuja wakati jiji hilo linakabiliwa na mfmuko wa uuzaji wa dawa za kulevya. Hata hivyo mtandao wa habari wa msnbc umesema baadhi ya wafanyakazi walioachishwa, huenda wakaitwa kazini tena, mambo ya fedha yatakapokaa sawa... Sijui lini lakini...

Mkulima wa bangi

Mkulima mmoja wa bangi kusini mwa California nchini Marekani, amemshitaki mwenye nyumba wake, kwa sababu zao lake lenye thamani ya dola elfu thelathini na tano limeibiwa ndani ya nyumba aliyokuwa akiishi.

Image caption Bangi

Bwana huyo Gary Hite ambaye amekodi nyumba kubwa kutoka kwa kampuni ya Hunco Way LLC, ameishitaki kampuni hiyo kwa uzembe na kukiuka mkataba. Amesema kampuni hiyo ilishindwa kutengeneza kitasa cha nyumba aliyopanga na kusababisha wezi kuingia na kuiba bangi aliyokuwa akipanda ndani ya nyumba hiyo. Bwana huyo aidha amejitetea kuwa alikuwa akipanda bangi hiyo kwa sababu za kiafya.

Shitaka hilo linaonesha mimea thelathini na mitano ya bangi iliibiwa, na kila mmoja ukiwa na thamani ya dola elfu moja. Hata hivyo mtandao wa msnbc umesema polisi wa huko wamesema shughuli za bwana Hite zilikuwa haramu.

Na kwa taarifa yako....

Na kwa taarifa yako............Watanzania wengi bado wanaamini kuwa wakipigiwa simu na namba isiyoonekana, au private number wanadhani wakipokea itawalipukia...

Jamani wabongo hakuna kitu kama hicho.....

Tukutane wiki ijayo .....panapo majaaliwa.

Habari kutoka mitandao mbalimbali ya habari duniani