Huwezi kusikiliza tena

Kisa na Mkasa na Salim Kikeke

Kondom zaziba vyoo

Baada ya michuano ya Jumuiya ya Madola kughubikwa na taarifa za wenyeji kutokuwa tayari, wiki moja baada ya michuano hiyo kuanza maelfu ya mipira ya kiume imesababisha mabomba ya maji kuziba mjini New Delhi.

Image caption Moja ya vyoo kabla ya mashindano kuanza

Mabomba hayo yameziba kutokana na mipira hiyo kutupwa vyooni. Mipira hiyo imetolewa bure kwa wanamichezo, ukiwa ni mpango wa kuhamaisha mapenzi salama, mpango ambao ulianza mwaka 1992, katika michuano ya olimpiki ya Barcelona. Gazeti la Mail la India limeripoti kuwa kuna mashine maalum imewekwa katika kijiji cha wanamichezo ambacho kina wanamichezo na viongozi wake wapatao elfu nne. Mwanzo wa michezo hiyo Mashine hiyo ilikuwa imewekwa pakiti elfu nne, ambapo kila pakiti ina mipira miwili.

Image caption Mike Fennell, rais wa michezo ya Commonwealth

Taarifa zimesema nusu ya idadi ya mipira hiyo ilikuwa imechukuliwa. Rais wa michuano ya Commonwelath Mike Fennell amewaambia waandishi wa habari kuwa mafundi bomba wanashughulikia kuzibua, mambomba yaliyoziba, na kuongeza kuwa, ni jambo zuri ikiwa wanamichezo wanazingatia mapenzi salama.

Hata hivyo afisa mmoja ambaye hakutaka kutajwa jina lake, ameliambia gazeti la Independent kuwa, hakuna mabomba yaliyoziba, na wala hakuna fundi aliyeitwa kuzibua, na kuwa huo ni uzushi tu wa vyombo vya habari.

Gundi ndani ya jicho

Mwanamama mmoja nchini Marekani, almanusura apoteze uwezo wake wa kuona, baada ya kutia gundi kwenye macho yake akidhani ni dawa ya macho.

Image caption Matho....

Mwanamama huyo, Irmgard Hol wa Arizona, amesema alifanya hivyo kwa kuwa chupa ya gundi na dawa ya macho zinafanana sana. Mama huyo, ambaye alifanyiwa matibabu ya macho mwaka mmoja uliopita amesema, mara moja alishituka kuwa, kuna tatizo baada ya matone kadhaa ya gundi kuingia jichoni mwake. Kwa mujibu wa kituo cha televisheni cha KSAZ, mwanamama huyo baada ya kufanya mkanganyiko huo mara moja alijaribu kuosha jicho lake kwa kutumia maji.

Image caption Chupuchupu kuwa chongo...

Hata hivyo, gundi aliyotumia ni ile ambayo huganda mara moja, na ndicho kilichotokea, na hivyo kuligandisha kabisa jicho lake na kushindwa kufunguka. Bi Irmgard alilazimika kwenda hospitali, na waganga nao kulazimika kuikata gundi hiyo ambayo tayari ilikuwa imeshika vilivyo, na baada ya kulifungua jicho, wakaosha gundi iliyosalia, ili isilete madhara zaidi.

Nguruwe wapendao reggae

Mfugaji Nguruwe mmoja nchini Rwanda anatengeneza nyama kiwango cha juu, kwa sababu anawapigia muziki.

Image caption Napenda sana R'n'B...

DJ huyo wa nguruwe, itwaye Edmund Ndizeye huwapigia nguruwe wake miondoko ya Hip Hop, reggae, RnB, nyimbo za mahaba, na hata nyimbo za kinyarwanda. Baada ya kuwalisha mifugo wake chakula Bwana Ndizeye huwapigia nyimbo laini kama zile za msanii Celine Dion au hata Bob Marley, ili wanyama hao wapumzike na baadaye huwapigia ngoma nzito nzito kama zile za Jay Z au Tupac, ili kuwachangamsha.

" Iwapo tunataka wapate uja uzito tunawapigia muziki mzito zaidi, ili madume wawe na nguvu na urijali" amesema kiongozi wa DJ Ndizeye, aitwaye Gerard Sina. Shirika la habari la reuters limesema Bosi Sina amesema aligundua mbinu hiyo wakati akiwa nchini Ubelgiji miaka sita iliyopita.

Image caption Kiti moto

Mfugaji huyo amesema ameshuhudia ufanisi mkubwa kwa kutumia nyimbo katika shamba lake lililopo Urwibutso, kaskazini mwa Rwanda. "Wanadamu wanapenda muziki, kwa hiyo nikajiuliza wanyama je?" amesema bwana Sina. Amesema njia hiyo iwapo itatumika na wafugaji wengine itasaidia kuondoa umasikini katika eneo hilo.

Labda kumpigia nguruwe reggae, si sawa na kumpigia mbuzi gitaa....

Uzalendo na wimbo wa taifa

Sheria mpya imepitishwa nchini Ufilipino, ambapo watu watakaoshindwa kuimba wimbo wa taifa watakabiliwa na adhabu ya kwenda jela. Bunge la nchi hiyo lililokaa katika mji mkuu, Manila, limepiga kura ya kupitisha muswada huo. Wabunge mia moja na tisini na sita walisema ndio na hakuna aliyeupinga muswada huo.

Image caption Ramani ya ilipo Ufilipino

Sheria hiyo inapiga marufuku kukosea kuimba Lupang Hinirang, ambao ni wimbo wa taifa na maana yake ni Nchi Niipendayo. Huku ikiwa imesalia maseneta tu kuupitisha kuswada huo, wale watakaokosea kuimba wimbo wa taifa hivi karibuni huenda wakajikuta wakienda jela na kupigwa faini ya zaidi ya dola elfu mbili za kimarekani.

Aidha upeperushaji wa bendera ya taifa kwa njia bila ya kuwa na uzalendo itakuwa kosa la jinai chini ya sheria hiyo mpya. Mwakilishi katika bunge Salvador Escudero, ambaye ndiye ametayarisha muswada huo amewaambia waandishi wa habari kuwa muswada huo unalenga kukuza utaifa. Gazeti la Metro la London limesema bwana Escuredo ametajwa kuwa amekuwa akikasirishwa na wanamuziki nchini Ufilipino kwa kubadili wimbo wa taifa na kwamba watu hubadili bendera ya taifa kutengeneza t-shirt na kaptura.

na kwa taarifa yako.... Kisa na Mkasa ni habari za kweli zinazotokea duniani kote....

Tukutane wiki ijayo.... Panapo majaaliwa....

Habari kutoka vyanzo mbalimbali kwenye mtandao