Huwezi kusikiliza tena

Kisa na Mkasa na Salim Kikeke

Akaanga kidole chake

Bwana mmoja nchini New Zealand, alikata kidole chake, na kukikaanga na kuongeza mboga mboga kisha akakila. Jarida ya kitabibu la Australasia Psychiarty limesema mtu huyo mwenye umri wa miaka 28, alikata kidole chake akiwa mzima bila hata kutumia dawa yoyote ya kuzuia maumivu au dawa za kulevya.

Image caption Jamaa alikula kidole chake...

Hata hivyo jarida hilo limesema mtu huyo, ambaye ametajwa kama bwana 'X' alikuwa akisumbuliwa na msongo wa mawazo, na hata wakati mwingine akifikiria kujiua.

Gazeti la New Zealand Herald likikariri jarida hilo limesema bwana huyo alitumia msumeno wa umeme kukata kidole chake, na kukiweka katika kikaango na kuanza kukaanga huku akiongeza mbogamboga ili kuongeza ladha.

Taarifa zinasema bwana huyo awali alipanga kukata vidole vingine vya mkono wake, baada ua kumaliza kukila cha kwanza. Hata hivyo alibadili mawazo, na kujutia jambo alilofanya akisema jambo hilo limemdhoofisha.

Ndege ndani ya gari

Polisi nchini Canada wanasema wamemkamata mwanamke mmoja akiendesha gari akiwa hajavaa nguo kikamilifu, huku akiwa na ndege ndani ya gari hiyo akirukaruka.

Haki miliki ya picha Other
Image caption Ndege kama huyu..

Polisi wa Kitchener, Ontario wamesema mwanamke huyo mwenye umri wa miaka hamsini na minane, alikamatwa baada ya polisi kumuona akiendesha gari, huku akipioga honi mfululizo.

Polisi walipatwa na wasiwasi na hali hiyo, na kujaribu kulisimamisha gari la mwanamama huyo. Mama huyo aligoma kusimamisha gari, lakini badala yake gari hilo lilikwenda kugonga basi la abiria, pamoja na gari jingine.

Baada ya ajali hiyo, ambapo hakuna aliyeumia polisi walimkamata mwanamama huyo.

Polisi wamesema mama huyo hakuwa akiendesha gari kwa kasi, na wala hakuwa amekunywa pombe. Haijafahamika kipi kilikuwa kimemsibu mwanamama huyo. Wanaharakati wa wanyama, walimchukua ndege aliyekuwa ndani ya gari, na mama huyo kupelekwa polisi.

Mtoto wa 20 na bado...

Mwanamama mmoja nchini Ukraine, amejifungua mtoto wake wa ishirini, na kuwa mwanamke aliyepata watoto wengi zaidi nchini humo. Shirika la habari la Xinhua limemkariri mwanamama huyo mwenye umri wa miaka arobaini na moja, akisema na hapo sio mwisho, bado ana mipango ya kupata watoto zaidi.

Image caption Mtoto mchanga

Madaktari wamesema mama huyo anaendelea vizuri na kichanga chake kipya, ambacho ni mtoto wa kiume. Familia ya mama huyo sasa ina watoto kumi wa kiume, na kumi wa kike, na wanaishi katika kijiji kimoja magharibi mwa Ukraine, kwa mujibu wa mtandao wa Ukranews.

Jonathan, mtoto wa kwanza wa mama huyo ana umri wa miaka ishirini, na tayari amekwisha oa. Watoto sita wa mama huyo wanafanya kazi, wanane bado wanasoma, huku wengine sita wakiwa bado katika shule ya chekechea.

Familia hiyo inamiliki shamba dogo ambalo watoto wao hufanya kazi hapo. Wazazi wa watoto hao wanasema wanawapa watoto elimu bora na kuwafunza kuheshimu utamaduni. Televisheni ni marufuku katika nyumba yao.

Mama mwenye rekodi kubwa zaidi ya kupata watoto wengi inashikiliwa na Leontina Albina kutoka Chile, ambaye alijifungua watoto hamsini na tano.

Akatalia jela

Mfungwa mmoja nchini Uchina, ameendelea kukiri makosa mengine ya uhalifu wakati akiwa gerezani, ili asiachiliwe huru. Kwa mujibu wa gazeti la jioni la Chingqing, Bwana huyo aitwaye Wang, mwenye umri wa miaka kumi na nane, alipewa hukumu ya kukaa gerezani kwa miaka mwili, mwezi uliopita, kwa kosa la kuiba fedha taslimu yuan elfu tatu, sawa na dola mia nne sitini pamoja na kuku.

Haki miliki ya picha c
Image caption Jela

Baada ya kuingia gerezani bwana Wang alianza kukiri makosa mengine aliyowahi kuyafanya zamani, na hivyo adhabu yake ya kukaa gerezani imeongezwa hadi miaka minne na nusu kutoka miwili.

Alipoulizwa na majaji, kwa nini anakiri mashitaka hayo, bwana Wang amesema hapendwi na familia yake, na kuwa anaona ni bora akae gerezani kuliko kurejea nyumbani kwao.

Mwizi juha

Mwizi mmmoja aliyekuwa akisakwa na polisi nchini Marekani, amejikuta akikimbilia kwa polisi bila ya mwenyewe kujijua.

Image caption Mwivi..

Polisi wa Salisbury, Massachussetts wamesema mtu huyo Joseph Dastous mwenye umri wa miaka ishirini na moja, ndio mwizi juha ambaye hawajapata kuona.

"Wezi huwakimbia polisi," amesema Richard Merill, mkuu wa polisi wa Salisbury, " Lakini kesi hii, sijawahi kuona katika miaka 33 katika kazi yangu-- kwamba mwizi ananikimbilia mimi, badala ya kunikimbia." amesema Kamanda Richard.

Taarifa zinasema mkasa ulianza baada ya kijana huyo kwenda kuiba gari katika shamba moja. Lakini hata hivyo wenye gari walimkurupusha na mara akaanza kutimua mbio.

Alikimbia hadi katika barabara kuu, na mara moja akaanza kusimamisha magari akiomba msaada. Kwa bahati mbaya, au nzuri gari aliyosimamisha ni ya mkuu wa polisi Richard Merill.

Gari hiyo haikuwa na alama zozote zinazoonesha kuwa ni ya polisi. Kijana huyo mara moja alifungua mlango wa gari na kukaa ndani, huku akimshurukuru aliyekuwa akidhani ni msamaria mwema.

"Ghafla akaniangalia na kusema, mbona kama nakufahamu vile" amesema kamanda Merrill, na kamanda huyo akamjibu "Lazima utakuwa unanifahamu, mimi ni mkuu wa polisi".

Na kwa Taarifa yako

.....Somalia ndio nchi pekee dunaini ambayo wananchi wake wote wanazungumza lugha moja tu.... Kisomali.

Nakutakia Pasaka Njema....

Tukutane wiki ijayo.... panapo majaaliwa...