Huwezi kusikiliza tena

Kisa na Mkasa na Salim Kikeke

Bora Punda?

Punda mmoja nchini Bulgaria amependekezwa kuwania nafasi ya umeya katika mji wa Varna.

Gazeti la Metro la hapa London limeripoti kuwa Punda huyo aitwaye Marco amechaguliwa na chama cha New Bulgaria kuwawakilisha katika uchaguzi.

Imeripotiwa kuwa chama hicho kimeona punda Marko ni mgombea muafaka kupambana na Meya aliyepo madarakani kwa sasa aitwaye Kiril Yordanov, ambaye wanahisi hafanyi kazi ya kuridhisha. Angel Dyankov, ambaye ni mkuu wa kampeni wa chama cha New Bulgaria amesema, tofauti na wagombea wengine wa umeya na wanasiasa, Punda wetu ana hadhi, sio mwizi, hasemi uongo na huhakikisha kazi inafanyika.

Mwanachama mwingine wa chama hicho Doychin Dimitriovmade naye ameonesha kutoridhishwa na meya wa sasa wa mji wa Varna.

"Maisha ya punda Marko yapo hatarini kwa kuwa maeneo mengi yenye majani sasa yameanza kupotea" amesema bwana Doychin. "Waache wananchi wa Varna wachague wenyewe nani anawafaa, kati ya punda na meya anayetetea kiti chake.

Mtoto mla balbu

Mtoto mmoja wa kike mwenye umri wa miaka mitatu hapa Uingereza ametafuna balbu.

Mtoto huyo Natalie Hayhurst, almanusura apoteze maisha yake baada ya kutafuna na kumeza vipande cha chupa ya balbu hiyo.

Mama wa mtoto huyo, Colleen ameliambia gazeti la Daily Mail kuwa, mara nyingi hapendi kula vioo tangu alipukula balbu hiyo, lakini hula zaidi matofali na vijiti vya miti. "Nimekuwa nikiwapigia simu wataalam wa sumu mara nyingi kuomba msaada kutokana na mwanangu huyu" amesema mama huyo.

Mtoto huyo anasumbuliwa na maradhi yaitwayo Pica, hali ambayo humfanya mtu kupenda kula vitu visivyo na virutubisho vyovyote. "Yaani anaweza kula kipande cha tofali kama vile mtu anavyokula chocolate" amesema mama huyo. Hajali ladha, uchungu au utamu.

Pesa chooni

Mtu mmoja asiyefahamika nchini Japan ameweka fedha taslimu takriban dola laki moja na elfu thelathini, katika choo cha umma.

Mtu huyo ametaka fedha hizo zitolewe kama msaada wa walioathirika na tetemeko la ardhi na tsunami lililotokea Japan mwezi Machi.

Fedha hizo ambazo zimewekwa vizuri katika mfuko wa plastiki, ziliachwa kwenye choo kinachotumiwa na jamii katika viunga vya jiji la Tokyo.

Fedha hizo pia zilikuwa na ujumbe usemao " Mimi ni mpweke na sizihitaji fedha hizi" Mamlaka za mji zimesema zitapeleka fedha hizo kwa shirika la msaklaba mwekundu, iwapo hakuna mtu atajitokeza kuzidai katika kipindi cha miezi mitatu.

Maafisa wa jiji wamesema mtu huyo aliingia kimya kimya na kutoka chooni humo bila mtu yeyote kumuona. Hii si mara ya kwanza, kwa mtu asiyefahamika nchini Japan kuacha kitita cha pesa chooni. Mwaka 2007, bahasha mia nne zikiwa na fedha zilikutwa zimewekwa katika vyoo mbalimbali nchini humo. Fedha hizo mara nyingi hupelekwa polisi, lakini hakuna watu wanaojitokeza kudai fedha hizo.

Mamilioni kimakosa

Mtu mmoja anayetuhumiwa kukimbia nchini New Zealand baada ya kuwekewa fedha kimakosa katika akaunti yake ya benki, amekamatwa nchini Hong Kong.

Bwana huyo, raia wa Uchina aliwekewa mamilioni ya dola kwenye akaunti yake kimakosa. Polisi wanasema bwana huyo anashikiliwa na polisi wa kimataifa, Interpol.

Kwa mujibu wa BBC, miaka miwili iliyopita, bwana huyo aliomba benki imuongeze fedha kidogo kama mkopo - overdraft - lakini benki kwa bahati mbaya, au nzuri wakamuwekea dola milioni saba na nusu.

Benki hiyo ilipogundua makosa hayo, lakini tayari kiasi kikubwa cha fedha kilikuwa kimekwisha hamishiwa katika akaunti nyingine.

Mhalifu kawa afisa magereza

Mtu mmoja aliyekuwa akisakwa na polisi nchini Uchina kwa muda mrefu, amekutwa akifanya kazi kama afisa wa magereza.

Gazeti la Beijing News limeripoti siku ya Alhamisi kuwa bwana huyo Wang Zhijia alikuwa anatuhumiwa kwa kosa la kumshambulia mke wake kwa tofali miaka kumi iliyopita.

Baada ya shitaka hilo kufikishwa polisi, bwana huyo alitoroka na haikujulikana yuko wapi. Polisi waligundua wiki hii kuwa mtu waliyekuwa wakimsaka kwa miaka kumi, anafanya kazi kama afisa wa magereza katika jimbo la mashariki la Anhui.

Na kwa taarifa yako.....Pilipili manga ndio kiungo maarufu zaidi duniani cha chakula..

Tukutane wiki ijayo... panapo majaaliwa..