Huwezi kusikiliza tena

Kisa na Mkasa na salim Kikeke

Msichana ageuka punda?

Bwana mmoja nchini Zimbabwe amedai kuwa kahaba aliyekuwa akifanya naye mapenzi amegeuka ghafla na kuwa punda.

Bwana huyo, Sunday Moyo ambaye amefikishwa mahakamani siku ya Jumatatu kwa kosa na kukutwa akifanya mapenzi na mnyama huyo amesema anampenda sana mpenzi wake huyo. Bwana Moyo aliiambia mahakama mjini Zvishavane kuwa huyo waliyemkuta naye sio punda bali ni mwanamke ambaye alikutana naye katika klabu ya usiku ya starehe.

Gazeti la Metro limesema polisi wa Zimbabwe wakiwa katika doria saa za alfajiri, walimkuta bwana huyo mwenye umri wa miaka 28, katika mji wa Mandava, akifanya mapenzi na punda nje ya nyumba yake. Mnyama huyo alikuwa amelala chini huku shingo yake ikiwa imefungwa kamba, na kamba hiyo kufungwa kwenye mti. Kwa mujibu wa mtandao wa New Zimbabwe.com bwana Moyo amekiri makosa ya kujamiiana na mnyama, lakini aliiambia mahakama kuwa "Mheshimiwa Jaji, niligundua tu kuwa ni mnyama, wakati polisi waliponikamata". Bwana huyo amesema alipata kahaba aliyekubali kulipwa dola ishirini, lakini amesema hafahamu ilikuwaje hadi akageuka na kuwa punda. "Lakini bado nampenda sana" amesema bwana Moyo. Bwana huyo ameswekwa rumande na kuamriwa kufanyiwa uchunguzi wa akili.

Mke arudi ghafla

Bwana mmoja aliyealika msichana nyumbani kwake, wakati mkewe hayupo, alimkana msichana huyo na kumuita mwizi, baada ya mkewe kurejea nyumbani ghafla.

Bwana huyo, Kevin Gaylor wa Colorado Springs Marekani, alikutana na msichana kwenye mtandao wa Craiglist.com na kumwambia aende kumtembelea nyumbani kwake. Hata hivyo mke wa bwana Kevin alirudi nyumbani ghafla, na kumfaya bwana huyo kupagawa asijue la kufanya.

Muda mfupi baada ya mke wake kuwasili, msichana aliyealikwa naye akafika. Kujaribu kuokoa jahazi bwana huyo alipiga simu polisi na kusema kuna mwizi nyumbani kwake. Gazeti la Metro limesema polisi watano walikwenda haraka nyumbani kwa bwana Kevin kupambana na mwizi ambaye waliambiwa alikuwa na silaha.

Badala yake polisi walikuta msichana mwenye umri wa miaka 20 akiwa nje ya nyumba ya bwana Kevin. Msichana huyo aliwaambia Polisi kuwa alisafiri kwa muda wa zaidi ya saa moja ili kukutana na Kevin, na kuwa walikuwa wakiwasiliana kwa muda wa wiki mbili kupitia simu na internet. Polisi walipogonga mlango wa bwana Kevin, alitoka na kuanza kuzungumza kwa sauti ya chini na kuwasihi polisi wamuondoe msichana huyo. Hata hivyo bwana huyo alikamatwa na kushtakiwa kwa kosa la kutoa taarifa za uongo kwa polisi.

Wezi waacha 'ushahidi' muhimu

Polisi nchini Sweden wamewakamata wezi wawili baada ya wezi hao kuacha haja kubwa karibu na mahala walipofanya wizi wao. Wezi hao walijisaidia nje ya nyumba moja katika eneo la Vara, katikati ya Sweden, muda mfupi kabla ya kuvunja nyumba na kufanya wizi.

Gazeti la huko limesema baada ya kuvunja nyumba hiyo walimkamata mwenye nyumba hiyo na kumfunga na kamba na kisha kujichukulia walichokuwa wakikitaka. Taarifa zinasema wezi hao waliiba fedha taslimu kronor elfu kumi, sawa na dola elfu moja na mia tano, pamoja na vifaa vingine na gari.

Mbali na kuhakikisha wanateketeza kila ushahidi ili wsikamatwe, walisahau kufukia kinyesi chao. Makachero katika upekuzi wao walikuta kinyesi hicho na waliweza kutumia teknolojia ya DNA na kuwatambua wezi hao. Mtandao wa habari wa Sweden umesema wezi hao waliweza kutambuliwa na hatimaye kukamatwa.

Bwana harusi mzee duniani

Bwana mmoja nchini India Hazil Abdul Noor, mwenye umri wa miaka mia moja na ishirini, ameweka historia wiki iliyopita, baada ya kufunga ndoa na mwanamke nusu ya umri wake.

Gazeti la Times of India limesema bwana huyo ambaye ni mjane, alifunga pingu za maisha na Samoi Bibi mwenye umri wa miaka sitini. Zaidi ya wageni mia tano walihudhuria harusi hiyo iliyofanyika katika kijiji cha Satgori, kilichopo kwenye jimbo la Assam.

Wageni zaidi ya mia moja walitoka upande wa bwana harusi, wakiwa ni pamoja na wanae wawili wa kiume, wanne wa kike, na watoto wao, na watoto wao, na watoto wao. "Haikuwa rahisi kumtafutia baba yetu mke" amesema mtoto wa kiume wa bwana harusi, akizungumza na gazeti la Times. "Hata hivyo kwa Kudra za Mungu, tumepata mama mpya, ingawa umri wake ni nusu ya wa baba yetu" amesema kijana huyo Hazi Azir. Bwana Noor anadhaniwa kuwa ndio bwana harusi mzee zaidi duniani.

Na Kwa taarifa yako........

Kwa wastani mwanamke huzungumza maneno elfu saba kwa siku, mwanaume huzungumza takriban maneno elfu mbili.....

----------------

Tukutane Wiki Ijayo...... Panapo Majaaliwa..

----------------

Taarifa kutoka mitandao mbalimbali ya habari duniani