Huwezi kusikiliza tena

Kisa na Mkasa na Salim Kikeke

Hamu ya TV

Image caption Flat screen kama hii

Bwana mmoja nchini Marekani amemakatwa baada ya kuvunja nyumba ya watu ili atazame TV na kupiga kinanda.

Bwana huyo Jason Bastrom wa mjini Oregon amedai kuwa mlango wa mbele wa nyumba hiyo ulikuwa wazi, na kulikuwa na jamvi mlangoni lililoandikwa 'karibu'.

Gazeti la Metro limesema mwenye nyumba ambaye alikuwa amelala wakati huo, ghafla alisikia sauti ya kinanda kikipigwa katika chumba kingine.

Huku akiwa na hali ya hofu, mwenye nyumba huyo Jamie McGowan alipiga simu polisi kuomba msaada. Jamie pia aliwaita majirani wake ambao walikuja na kumkuta mtu huyo akitazama TV. Polisi walipowasili walimchukua na kumpeleka korokoroni. Taarifa zinasema ingawa mtu huyo alikuwa hana nia ya kufanya wizi wowote bali kutazama TV na kupiga kinanda, ameshtakiwa kwa kosa la kuingilia faragha ya mtu.

Wapora mkate

Haki miliki ya picha SPL
Image caption Sandwich kama hii

Watu wawili nchini Marekani wameshtakiwa kwa tuhuma za kumuibia chakula mtoto mwenye umri wa miaka kumi na mitatu.

Mtandao wa cnews.com umesema kijana huyo alikuwa akitembea kwenda nyumbani baada ya kununua kipande cha mkate, sandwich. Taarifa zinasema ghafla watu wawili walisimamisha gari na kumfuata kijana huyo. Mmoja wa wawili hao alimtishia kijana huyo kwa bunduki na kumwambia "Simama hapo hapo". Mwingine alianza kumsachi mifukoni kijana huyo, na wawili hao walipoona kuwa hana fedha mfukoni, walimnyanganya mkate wake na kukimbilia katika gari lao.

Hata hivyo wezi hao, hawakuchukua simu ya kijana huyo, na mara moja kijana huyo alitumia simu hiyo kuita polisi. Polisi waliitikia witi huo haraka na kuwakamata wezi hao wakiwa na wenzao wengine wawili, na wote wameshtakiwa.

Foleni ya magari tafrani

Image caption Msongamano wa magari

Majambazi watano nchini India wametumia tatizo la foleni ya magari barabarani kutoroka kutoka ndani ya karandinga siku ya Jumanne.

Gazeti la Times of India limesema majambazi hao walikuwa wakipelekwa katika gereza la Dum Dum wakitokea katika mahakama ya Barasat mjini Calcutta. Tukio hilo lilitokea saa moja na nusu jioni wakati karandinga hilo lilipokwama kwenye msongamano wa magari barabarani.

Gazeti hilo limekaririwa likisema majambazo hao walitoroka baada ya kufumua sakafu ya gari na kutorokea chini ya karandinga hilo.

Amri ya kufanyika kwa uchunguzi imetolewa, kutafuta kufahamu jinsi majambazi hao walivyoweza kutoroka, hasa ukizingatia kulikuwa na polisi wawili waliokuwa wakiwasindikiza. Bado haifahamiki iwapo majambazi hao walikuwa wamefungwa pingu au la. Watu walishuhudia majambazi hao wakikimbia kutoka katika karandinga hilo katika barabara ya Jesore na watu wengi wakiwa na mshangao waliamua kuwataarifu polisi. Taarifa ya tahadhari imetolewa katika vituo mbalimbali vya polisi ili kusaidia kuwakamata watoro hao.

Dereva azidiwa kasi na mwanaye

Dereva bingwa wa mbio za magari nchini Sweden anayefahamika kwa kuendesha gari kwa kasi, alishindwa kumwahisha mkewe mja mzito hospitali, na hivyo mtoto wao kuzaliwa ndani ya gari wakiwa njiani.

Mke wa dereva huyo Per Gunner Andersson alipatwa na uchungu wa uzazi usiku wa manane, siku ya Ijumaa, na wakalazimika kwenda hospitali kwa kutumia gari yao aina ya BMW.

Bwana Andersson akiendesha kwa kasi yake, alizidiwa kasi na mwanaye. Wakiwa njiani, wawili hao waliona hawawezi kuwahi hispitali, na hivyo kusimamisha gari lao na kupiga simu kuomba msaada wa hospitali. "Nilikuwa mtulivu kabisa" amesema Andersson akizungumza na gazeti la kwenye mtandao la Expressen. Gari la wagongwa liliwasili muda mfupi tu kabla ya mke wa dereva huyo kujifungua mtoto wa kiume.

Kutokana na panda shuka hiyo, dereva huyo amesema huenda mwanaye pia akawa dereva wa magari ya mashindano. Andersson alikuwa bingwa wa dunia wa mbio za magari kwa vijana mwaka 2004 na 2007.

Na kwa taarifa yako....

Unaweza kuwasha moto kwa kutumia kipande cha barafu

--------------

Tukutane wiki ijayo... panapo majaaliwa