Huwezi kusikiliza tena

Kisa na Mkasa na Salim Kikeke

Jambazi lajipiga risasi kwa wasiwasi

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Jambazi lajipiga risasi

Jambazi mmoja aliyeingia benki kuiba fedha, akiwa na wenzake, alifanikiwa kupora dola takriban elfu kumi na sita, lakini kutokana na wasiwasi akajipiga risasi mweyewe.

Picha za video katika kamera za usalama katika beki moja iliyopo Parana kaskazini, nchini Brazil imeonesha wezi watatu wakiwa na silaha wakiingia katika benki hiyo siku ya Jumatatu.

Kila kitu kilionekana kwenda kama kilivyopangwa, baada ya wezi hao kuwadhibiti walinzi wa benki na kufanikiwa kupora reais elfu thelathini za Brazil, sawa na dola elfu kumi na sita.

Hata hivyo mmoja wa majambazi hao, aliyekuwa mlangoni, alionekana akiwa na hali ya wasiwasi muda wote wakati wizi unaendelea. Mwizi huyo akiwa ameshika bastola mbili alionekana kutokuwa na hali ya utulivu kabisa, na ghafla ulisikika mlio.

Kutaharuki jambazi huyo alikuwa kajipiga risasi mwenyewe mguuni. Picha za CCTV zilionesha jambazi huyo akiondoka eneo la tukio huku akichechemea - OUCH - mguu wake alioujeruhi mwenyewe, huku wenzake wawili wakimtangulia kwa kasi.

Siku iliyofuata, jambazi huyo alikamatwa baada ya kwenda hospitali kutafuta matibabu, katika hospitali iliyo karibu na benki waliofanya wizi wao. Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Brazil, majambazi sita walihusika na wizi huo, lakini ni huyo mmoja tu aliyejipiga risasi mwenyewe ndio amekamatwa.

Sio mimi ni jini

Bwana mmoja nchini Marekani aliyekamatwa kwa mashtaka ya kumpiga mke wake, amewaambia polisi sio yeye alifanya hivyo bali ni majini.

Bwana huyo, Michael West kutoka mji wa Wisconsin, alishtakiwa wiki hii kwa kumkaba, kumpiga kumtukana mke wake na pia kuzuia polisi kufanya kazi yao, limeripoti gazeti la Oshkosh Northwestern. Bwana huyo alikamatwa baada ya majirani kuita polisi baada ya kusikia zogo, na polisi kukuta mwanamke akiwa na majeraha na damu huku akilia na kuomba msaada.

Polisi wamesema mwanamke huyo, ambaye ni mke wa Bwana Michael, aliwaambia kuwa mume wake alimpiga mangumi na kumkaba koo wakati wakizozana kuhusiana na masuala ya matumizi ya fedha.

Lakini polisi waliambiwa na mume huyo kuwa mke wake alipatwa na majeraha hayo kutokana na kuanguka. Alipoulizwa zaidi, bwana Michael alisema, "Kuna jini lilitokea na kumkaba mke wangu" limeripoti gazeti la Notrhwestern kwa kumkariri bwana huyo.

Akatalia jela

Image caption Jamaa agoma kutoka 'ndani'

Bwana mmoja nchini Marekani ameshtakiwa baada ya kugoma kutoka jela. Gazeti la Arizona Daily Sun limesema bwana huyo alikamatwa wiki iliyopita kwa kosa la kuingia eneo lililopigwa marufuku, lakini alitakiwa kuachiliwa huru siku ya Jumatatu baada ya kutambua kosa lake.

Hata hivyo, bwana huyo aitwaye Martin Batieni Kombate, aligoma kutoka katika jela ya wilaya ya Coconino.

Maafisa wa polisi walipofika kumwambia kuwa yuko huyo na kumtaka atoke jela, bwana Martin alisema, hana mpango wowote wa kutoka kizuizini humo. Aidha polisi zaidi walipoitwa kutaka kufahamu kwa nini hataki kutoka jela, bwana huyo alisingizia kuwa hataondoka selo kwa sababu amepoteza pochi yake. Licha ya maafisa wa polisi kuendelea kumweleza kuwa sasa yuko huru, bwana Martin alikataa kata kata kutoka jela, hata baada ya kubembelezwa mara kadhaa.

Mtoto aiba gari la baba

Mtoto mmoja wa miaka kumi nchini Ufaransa anashikiliwa na polisi, baada ya kuchukua gari la baba yake na kujaribu kwenda nalo shuleni kwao, baada ya kuachwa na basi la shule.

Kijana huyo, ambaye alimpakiza mwenzake mwenue umri wa miaka tisa, na ambaye pia alikuwa ameachwa na basi la shule, walifanikiwa kuendesha gari hilo kwa umbali wa kilomita mbili, kabla ya kugonga ukingo wa barabara, wameripoti polisi wa mji wa Valence.

"Nilikuwa nimevaa mkanda" amejitetea kijana huyo baada ya polisi kuwasili eneo la tukio. Vijana hao hawakuumia. Polisi wamesema kijana huyo huenda akashtakiwa kwa kosa la kuendesha gari bila ya kuwa na leseni, na kuharibu barabara ya umma.

Lakini waendesha mashtaka watafanya uamuzi kuona kama wafungue kesi au la.

Kagame ataka Wenger aondoke

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Arsene Wenger asema mashabiki wamuamini

Rais wa Rwanda Paul Kagame amemtaka kocha wa klabu ya soka ya Arsenal, Arsene Wenger kuachia ngazi.

Kagame ni shabiki mkubwa wa klabu hiyo yenye makao yake kaskazini mwa jiji la London. Rais Kagame amempiga kigongo hicho Mfaransa Wenger baada ya Arsenal kuchapwa mabao mawili kwa moja dhidi ya Manchester United wiki iliyopita.

Huo ulikuwa mchezo wa tatu kwa Arsenal kupoteza mfululizo. "Naipenda sana Arsenal, lakini kusema kweli Wenger anahitaji kufundisha timu nyingine, na Arsenal inahitaji kocha mwingine" amekaririwa Kagame kupitia mtandao wa Twitter. Gazeti la Sun la hapa Uingereza limesema Rais huyo amesema wakati sasa umewadia kwa klabu hiyo kufanya mabadiliko.

Wenger amekuwa kocha wa Arsenal tangu mwaka 1996, na mara ya miwsho kushinda kombe lolote ilikuwa mwaka 2005.

Na kwa taarifa yako.......

Farasi anaweza kulala usingizi akiwa amesimama

-------------

Tukutane wiki ijayo, panapo majaaliwa...

Habari na taarifa kutoka mitandao mbalimbali duniani