Huwezi kusikiliza tena

Kisa na Mkasa na Salim Kikeke

WEZI WAISHIO JELA

Haki miliki ya picha RIA Novosti
Image caption Jamaa wakiiba wanarudi ndani

Polisi na maafisa nchini Australia wanafanya uchunguzi kuhusu madai kuwa wafungwa wawili wanatoroka gerezani na kuingia mitaani kufanya uhalifu na kisha kurejea tena gerezani kimya kimya.

Uchunguzi huo umeanzishwa baada ya watu wawili wakiwa wamevaa sare za magereza kuingia katika duka moja karibu na mji wa Bathurst na kuiba kiasi kidogo cha fedha.

Gari la rangi nyeupe aina ya Toyota HiLux 4x4 ambalo walionekana wakiendesha wezi hao lilikutwa limetelekezwa saa kadhaa baadaye karibu na gereza la Oberon.

Gari hilo lilikuwa limeibiwa mapema mwezi uliopita, na hivyo kuzua hofu kuwa wezi hao wana tabia ya kutoroka na kurejea gerezani.

Mkulima mmoja naye amesema alikuta nyumba yake imevunjwa na vitu kuibiwa. Mtandao wa couriermail.com umesema polisi wametoa taarifa ikisema uchunguzi unafanyika kuhusiana na matukio hayo, na kuona kama wataendelea au hawataendelea.

UKAME WAATHIRI HADI BANGI

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Ukosefu wa mvua umesababisha ukame

Hali ya ukame imekumba eneo la kaskazini mwa Mexico kiasi kwamba imeathiri hadi kilimo haramu cha bangi na opium poppies zinazotumika kutengenezea dawa za kulevya.

Kwa mujibu wa kamanda wa kijeshi wa Mexico, Jenerali Pedro Gurrola ukosefu wa mvua umesababisha kilimo cha bangi kudorora kwa kiasi kikubwa.

Gurrola amesema uchunguzi wao umegundua mashamba machache ikilinganishwa na miaka iliyopita. "Huwa tunaona bangi nyingi" kamanda huyo amewaambia waandishi wa habari "kama mnavyoona hali ni kavu sana" amesema kamanda Gurrola.

Hata hivyo amesema wakulima hao wanatafuta mbinu nyingine kama vile kupanda karibu na mito au kufanya kilimo cha umwagiliaji maji kwa kutumia pampu.

SHULE ZA KUSOMA NYOTA

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Nani kaona... watoto wanasomwa viganja

Shule kadhaa za chekechea nchini Uchina zinatoza wazazi karibu dola mia mbili ili kusoma viganja vya watoto na kubashiri kama watoto hao watakuwa na mafanikio katika maisha yao.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Xinhua, wazazi wengi wanakimbilia kuwapeleka watoto wao kufanyiwa vipimo hivyo katika jimbo la kaskazini la Shanxi. Taarifa hiyo imesema watoto wanaopelekwa kusomwa viganja ni kuanzia wenye umri wa miezi mitatu.

Kwa mujibu wa kampuni inayoendesha usomaji wa viganja iitwayo Shanxi Daomeng Communication, usomaji wa viganja unangamua ujanja na vipaji vya watoto.

Hata hivyo baadhi ya wataalam wametupilia mbali teknolojia hiyo ya kusoma viganja vya mikono. "Teknolojia hii inabakia kuwa bila ushahidi" Xinhua imemkariri mtaalam mmoja.

Utabiri na ubashiri, ikiwa ni pamoja na kusoma viganja vya mikono ya watu una mizizi ya muda mrefu katika utamaduni wa Uchina, ingawa viongozi wa nchi hiyo wamekuwa wakiwakata wananchi kutofuatilia na hata kutoa adhabu kali kwa watu wanaofanya shughuli hizo.

Watu wengi, ikiwa ni pamoja na maafisa wa serikali hutafuta ushauri wa wataalam wa kusoma nyota, umeripoti mtandao wa cnews.com.

ATAKA LIKIZO JELA

Haki miliki ya picha AP
Image caption Angependa kwenda mahala kama hapa kupumzika

Mwanamama mmoja mwenye umri wa miaka thelathini na moja anayetumikia adhabu ya maisha jela nchini Sweden, amedai apewe likizo kutokana na kazi anayofanya gerezani humo.

Mtandao wa UPI.com umesema mwanamama huyo Natalia Pshenkina alifungwa kwa kukutwa na hatia ya kumuua rafiki wake wa kiume mwaka 2005.

Natalia alipatiwa kazi katika gereza la Ystad mwaka 2010 na anaamini anahitaji kupewa likizo yenye malipo, kwa mujibu wa sheria za kazi za Sweden, limeripoti gazeti la The Local.

Bi Natalia alimuandikia kansela wa sheria wa Sweden akiwasilisha malalamiko yake, inagwa alijibiwa kuwa hakuna likizo kwa wafungwa. Msemaji wa magereza wa Sweden, Anders Annerfalk amesema wafungwa wanaofanya kazi ndani ya magereza hawalindwi na sheria zinazowalinda wafanyakazi wengine.

"Kwa maana hiyo hakuna likizo" amesema.

WAFUNGWA WASHONA MIDOMO

Image caption Wajishona midomo

Zaidi ya wafungwa elfu moja nchini Kyrgistan wameshona midomo yao, kupinga hali mbaya za magereza.

Hata hivyo mamlaka za huko zinasema magenge ya uhalifu ndio yanachochea hali hiyo ili waweze kutoroka gerezani.

Kyrgistan ni nchi iliyokuwa chini ya utawala wa kisovieti, na ina wananchi milioni tano, na wafungwa elfu saba na mia sita. Kwa miaka mingi kumekuwa na matendo yanayofanywa na wafungwa, lakini hili la Jumamosi iliyopita lilizidi kiwango.

Kwanza wafungwa wengi walifanya mgomo wa siku kumi wa kula. Lakini hatua ya kuishona midomo yao imekuwa ya kipekee kiasi cha kutikisa maafisa wa magereza.

Mwandishi mmoja wa habari wa AP alishuhudia baadhi ya wafungwa wakiwa wamejishona midomo huku wakiwa wamebakiza tundu dogo tu la kupitishia maji. Wafungwa hao wametumia nyuzi ngumu na hata waya kujishona.

Na kwa taarifa yako......

Bara pekee duniani lisilo na nyoka ni Antarctica

Tukutane wiki ijayo.... panapo Majaaliwa....

Taarifa kutoka mitandao mbalimbali ya habari duniani.