Huwezi kusikiliza tena

Kisa na Mkasa na Salim Kikeke

Mwizi haachi asili

Haki miliki ya picha AP
Image caption Kompyuta kama hii

Mwizi mmoja hapa Uingereza aliyetakiwa na polisi kwenda kuomba msamaha kwa mtu aliyemuibia, alipatwa na kishawishi cha kumuibia tena baada ya kusamehewa.

Mwizi huyo Ivan Barker alikwenda nyumbani kwa Jacque Mathley kumuomba radhi kwa kumuibia kompyuta yake na pakiti kadhaa za sigara miezi mitatu iliyopita.

Baada ya Bwana Mathley kuona mwizi wake amekiri kosa na ni mnyenyekevu alimkaribisha ndani kwake.

Gazeti la Daily Mail limesema mwizi huyo alipoingia ndani alikuta bwana Mathley amenunua kompyuta nyingine. Baada ya mazungumzo marefu, bwana Mathley alitoka kwenda msalani, huku nyumba mwizi Ivan akaamua kuiba tena kompyuta na sigara na kutokomea. "Yaani kurejea sikuikuta kompyuta yangu" amesema bwana Mathley.

Mwizi huyo alikamatwa baadaye na polisi. Akiwa korokoroni mwizi huyo amesema kwa hakika alikuwa amekwenda kuomba msamaha kwa dhati kabisa, lakini alishinda kujizuia kufanya tena wizi.

Mwanamke akana kubaka

Haki miliki ya picha none
Image caption Mwanamama aliingia kwa kunyata

Mwanamama mmoja nchini Australia amefikishwa kizimbani kwa tuhuma za kumbaka mwanaume.

Gazeti la Daily Mail limesema mwanamama huyo Helen Elder alivunja mlango na kuingia katika nyumba ya mwanaume mmoja ambaye hakutajwa jina kwa sababu za kisheria, na kisha kumbaka.

Mwanamama huyo mwenye umri wa miaka thelathini na tisa amefikishwa katika mahakama ya wilaya ya Adelaide na kusomewa mashtaka ya kuingia katika nyumba ya mtu kinyume cha sheria na kubaka.

Upande wa mashtaka umesema mwanamke huyo aliingia katika nyumba ya bwana huyo aliyekuwa amelala, na kisha kumuamsha na kumlazimisha kufanya vitendo ambavyo hakuwa tayari kuvifanya.

Mshtakiwa huyo amekana mashtaka yote.

Matatani kwa kumlewesha mbwa

Image caption Ni kosa kumlewesha mbwa

Bwana mmoja nchini Marekani amekamatwa na polisi baada ya kumpa pombe mbwa wake na kumlewesha kiasi cha mbwa huyo kushindwa hata kutembea.

Bwana huyo Todd Harold Schreiner, anashtakiwa kwa kosa la kutesa wanyama. Polisi wa mji wa East Helena walikuta mbwa huyo akiwa amelewa chakari, mara nne zaidi ya kipimo cha wanadamu kinachoruhusu kuendesha gari.

Taarifa zinasema mbwa huyo aitwaye Arly II wakuweza kusimama au kutembea vyema wakati alipokutwa na polisi ndani ya baa moja saa tano na nusu usiku.

Mbwa huyo alichukuliwa na kupelekwa katika zahanati ya wanyama ambapo vipimo vilionesha ana ulevi wa asilimia sifuri nukta tatu nne nane katika damu yake.

Kisheria kipimo cha mwisho cha ulevi wanaadamu wanaruhusiwa kuwa nacho na kuendesha gari ni asilimia sifuri nukta sifuri nane. Muuzaji katka baa aliyokutwa mbwa huyo amesema mwenye mbwa alimpa mbwa wake kilevi aina ya vodka.

Fahali maarufu afariki

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Fahali

Ngombe dume ambaye ametoa mbegu za kuzaliwa kwa maelfu ya ngombe wanaotoa maziwa kwa wingi duniani, amefariki dunia nchini Ufaransa, akiwa na umri wa miaka ishirini na saba.

Fahali hilo lijulikanalo kwa jina la Jacko linadhaniwa kutoa mbegu kwa ngombe, na kuzalisha jamii ya ndama takriban laki nne ambao sasa ni ngombe wanaotoa maziwa kwa wingi.

Katika maisha yake pia, fahali Jacko anadaiwa kutoa dozi milioni 1 nukta saba ya mbegu zake ambazo zilisambazwa katika nchi sitini duniani kote.

Rasmi fahali Jacko alizalisha ndama wa kike laki moja sitini na moja elfu mia nane themanini na nane. Mtandao wa News.com umesema hata hivyo nchi nyingine ambako mbegu zake zilipelekwa, hakukuwa na takwimu zozote rasmi zilizowekwa.

Taarifa zinasema kwa heshima yake, mwili wa ngombe dume huyo hautafanywa nyama kama ilivyo kawaida, badala yake mzoga wake utapelekwa katika jumba la makumbusho ya historia za asili mjini Paris.

Mti wakasirika kukatwa

Bwana mmoja aliyekuwa na wasiwasi kuwa mti mkubwa ulioota mbele ya nyumba yake huenda ukaanguka na kuvunja nyumba, aliamua, kuukata mti huo. Bwana huyo alitumia siku nzima kuukata mti huo kwa kutumia shoka, lakini mti huo ukaishia kuanguka juu ya nyumba yake na kuivunjilia mbali.

Picha za video zinazoonesha sakata hilo zimesambazwa kwenye wavuti wa you tube na kutazamwa na mamia ya watu. Picha inaonesha jinsi bwana huyo anavyojitahidi kuukata mti, bila kufuata misingi ya kukata mti, na jinsi mti unavyodondoka moja kwa moja juu ya paa ya nyumba.

Mtu huyo ambaye haijulikani yuko nci gain ana sikika akisema "ooh nyumba yangu…. Ooh chumbani kwangu" Hakuna taarifa zozote za mtu kuumia katika sakata hilo.

Na kwa taarifa yako .. Katika maisha ya binaadam kawaida, kwa wastani ataota nywele urefu wa karibu maili mia sita.

Tukutane wiki ijayo… panapo majaaliwa.