Huwezi kusikiliza tena

Kisa na Mkasa na Salim Kikeke

MFUNGWA AVAA GAUNI KUTOROKA

Image caption Viatu virefu sio jambo la mchezo

Mfungwa mmoja wa kiume nchini Brazil aliyekuwa akijaribu kutoroka gerezani kwa kuvaa nguo za kike amekamatwa tena na kurejeshwa ndani.

Bwana huyo Ronaldo Silva alinyoa nywele zake za mikononi na miguuni na kutoka kupitia lango kuu la gereza akiwa amevaa gauni la bluu, wigi kicwhani na viatu virefu.

Hata hivyo bwana huyo ambaye amefungwa kwa makosa ya uuzaji dawa za kulevya, alishtukiwa na polisi mmoja aliyeona akitembea tofauti na wanawake wengine mitaani.

Polisi wamesema nguo hizo aliletewa gerezani na mke wake. Mbali na kuvalia gauni hilo na viatu virefu Ronaldo pia alikuwa amepaka rangi ya mdomo-- lipstik nyekundu iliyokolea.

Polisi walimkamata dakika thelathini tu baada ya kufanikiwa kutoroka gerezani kutokana na kushindwa kutembea vyema na high heels. Mkurugenzi wa gereza hilo Carlos Welber amesema mke wake amekiri kumletea mume wake nguo za kike, lakini amesema hakufahamu kwa nini mume huyo alizitaka.

Mfungwa huyo alikuwa ndio kwanza tu amehamishiwa katika gereza hilo, baada ya kufanya jaribio la kutoroka katika gereza alilofungiwa awali.

MNYONYESHAJI ASIYEJULIKANA

Haki miliki ya picha bbc
Image caption Mama kwa mshangao...

Mama mmoja nchini Marekani alipatwa na mshituko baada ya kukuta mtoto wake mchanga akinyonyeshwa ndani ya nyumba yake na mwanamke asiyemfahamu.

Kituo cha radio cha KJJQ cha South Dakota kimesema mama huyo alipatwa na mshangao huo saa kumi na moja alfajiri alipokuta kichanga chake cha miezi miwili kikinyonyeshwa na mwanamama asiyefahamika.

Mama huyo alipiga simu mara moja polisi kuripoti suala hilo.

Aidha mama huyo alimchukua mwanaye, lakini mwanamama aliyekuwa akimyonyesha aliendelea kubaki ndani ya nyumba hiyo, hadi polisi walipowasili na kumkamata.

Jitihada za waandishi wa habari kutafa kufahamu zaidi kilichotokea ziligonga mwamba baada ya polisi wa kituo cha Brookings kutopokea simu, umeripoti mtandao wa Huffington Post. Hata hivyo taarifa zinasema mwanamke mwenye umri wa miaka ishirini na nne ameshtakiwa kwa kosa la kuingia katika nyumba isiyo yake kinyume cha sheria. Pia majina ya wakinamama hao na hata kichanga hayakuweza kupatikana mara moja.

MLEGEZO WAMPELEKA JELA

Haki miliki ya picha all voices
Image caption Mlegezo wampeleka jela siku tatu

Kijana mmoja mwenye umri wa miaka ishirni nchini Marekani amehukumiwa kwenda jela kwa siku tatu kwa kuvaa suruali yake chini ya kiuno, yaani mlegezo.

Jaji katika mahakama mjini Alabama alitoa adhabu hiyo kwa kijana aliyekuwa amevaa suruali aina ya jeans kwa misingi ya kukiuka maadili ya mahakama.

Kijana huyo LaMarcus D Ramsey alikuwa amefikishwa katika mahakama ya Autagua kwa kosa la kufanya wizi, limeripoti gazeti la Montgomery Advertiser.

Taarifa zinasema wakati kesi yake ikisikilizwa jaji John Bush alionekana kutatizwa sana na jinsi kijana huyo alivyokuwa amevaa suruali yake, na mara moja alitoa ari kijana huyo kupelekwa jela kwa siku tatu kwa kosa la kuvaa suruali mlegezo, au sag.

"Unadhalilisha mahakama kwa kuonesha makalio yako" amesema jaji huyo. Hali kadhalika jaji huyo amesema mbali na kukaa jela kwa siku tatu, akitoka, kijana huyo ametakiwa kununua suruali inayomtosha, au anunue mkanda, ili nguo yake ya ndani na makalio yake visionekane.

MFUNGWA AMN'GATA AFISA MAGEREZA

Image caption Kasheshe gerezani

Mfungwa mmoja wa kike nchini Marekani anakabiliwa na mashtaka zaidi, baada ya kumngata afisa wa magereza, siku ya jumatatu hadi meno yake mawili kun'gooka.

Mfungwa huyo Erin Babich, alikuwa akitumikia kifungo katika gereza la Manatee, karibu kilomita hamsini kusini mwa Tampa, Florida. Mtandao wa Big Pond News umesema mtafaruku ulianza baada ya Bi Babich kugoma kusikiliza mari za gereza na kujaribu kumpiga afisa mmoja wa gereza.

Wakati akifanya fujo hizo, maafisa wengine wa magereza walijitokeza kusadia, na ndipo alipoamua kumgnata mmoja wao mkononi kwa nguvu mno kiasi kwamba meno yake mawili yalingooka.

Bi Babich sasa ameshtakiwa kwa kosa la kumshambulia afisa wa magereza. Afisa aliyengatwa anapatiwa matibabu katika hospitali ya mji huo.

POLISI ASIYEJUA KUTUMIA BUNDUKI

Haki miliki ya picha afp
Image caption Shabaha sifuri

Mkuu wa Polisi wa mji mmoja nchini Marekani amepigwa marufuku kubeba bunduki kwa sababu hawezi kulenga shabaha inavyotakiwa.

Mtandao wa Huff Post umesema mkuu huyo Thomas Bennett amepunguziwa majukumu yake ya upolisi baada ya kufeli mtihani wake wa kulenga shabaha hivi karibuni.

Hatua hiyo inamaanisha polisi huyo haruhusiwi kuwasha taa za kimulimuli za gari ya polisi (SIRENS) na pia hata kusimamisha magari ya raia kwa ajili ya ukaguzi wa kawaida wa barabarani.

Hata hivyo Polisi Bennett mwenyewe amedai kuwa bado nana uwezo wa kutekeleza majukumu yake kama kawaida. Afisa mtendaji wa mji huo wa North Carolina Gregg Whitehead amesema bwana Bennett ametakiwa kujiandaa kufanya majaribio mengine tena ya kulenga shabaha kama inayotakiwa kipolisi.

Na kwa taarifa yako......Kuna takriban nywele mia tano hamsini katika kila nyusi za binaadam.

Tukutane wiki ijayo..... panapo majaaliwa...