Huwezi kusikiliza tena

Kalume afuata nyayo

Image caption Kalume akicheza marimba

Kalume Katana ni kijana aliyezaliwa tarehe mosi, mwezi Agosti mwaka 2002, na kuanza kuonyesha hisia za kucheza muziki tangu akiwa na umri mdogo sana.

Babake, John Katana Harrison, wa bendi ya Them Mushrooms nchini Kenya, anasema "Kalume alipenda kuchezea ala za muziki tangu akiwa mtoto kabisa, badala ya kuchezea vitu vinginevyo vya watoto kama ilivyo desturi".

Image caption Kalume akicheza gitaa

"Nakumbuka wakati mmoja alipokuwa mtoto wa miaka miwili u nusu, na nilipoandamana naye hadi kwa mazoezi ya muziki kwa mara ya kwanza, na kamwe hakutaka kuondoka, hadi tulipomaliza mazoezi", alielezea John.

Kwa kumtizama baba na wajomba wakicheza muziki, Kalume alianza kutamani kucheza muziki, na mara kwa mara akishirikiana na baba alipokuwa katika hali ya kufanya mazoezi, na hasa nyakati shule zilipofungwa, akiwa mapumzikoni.

Kalume sio tu hufurahi kucheza muziki, bali utaratibu mzima unaohusika na utunzi, hata shughuli zote za kurekodi muziki.

Kwa kutoa rekodi yake ya kwanza ya "Tujivunie timu zetu" akiwa anaelekea kufikia umri wa miaka 10 mwezi Agosti, bila shaka atakuwa na miaka mingi ya kuimarisha muziki wake na kuufanya kuwa burudani safi.