Huwezi kusikiliza tena

Kisa na Mkasa na Salim Kikeke

Nipige risasi tafadhali...

Mamlaka nchini marekani zinasema bwana mmoja mjini New York alimshawishi rafiki yake ampige risasi kwa sababu alitaka kufahamu mtu anajisikiaje anapopigwa risasi.

Polisi katika eneo la St Lawrence wamesema tukio hilo lilitokea saa kumi na moja jioni siku ya Jumapili katika mji mdogo uitwao Stockholm.

Habari zinasema bwana Shawn Mossow wa mji wa jirani wa Norfolk alishawishiwa na rafiki yake ampige risasi. Rafiki yake huyo ambaye hakutajwa jina na polisi, inadaiwa alimbembeleza sana rafiki yake huyo ampige risasi kwa sababu alikuwa na hamu sana ya kuona jinsi watu wanavyojisikia wanapopigwa risasi. Rafiki yake huyo hatimaye alishawishika na kuamua kumpiga risasi mguuni rafiki yake huyo.

Habari zinasema alipigwa risasi mguuni, na amepelekwa hospitali na anatarajiwa kupona. Rafiki wa bwana huyo aliyefyatua risasi, ameshtakiwa kwa kosa la kufanya uzembe na anashilikiliwa na polisi. Aidha mtu aliyepigwa risasi hajasema alijisikiaje.

Haja yaua samaki

Waogeleaji katika ziwa moja nchini Ujerumani wamesababisha vifo vya samaki wanaoishi ndani ya ziwa hilo, kutokana na kujisaidia haja ndogo wakati wakiogelea.

Vifo vya samaki wengi vimetokea katika wiki mbilizi zilizopita katika ziwa Eichbaum, katika mji wa Hamburd, vimeripoti vyombo vya habari vya huko. Taarifa zinasema samaki wapatao mia tano wamekufa katika wiki mbili zilizopita.

Habaari zaidi zinasema mkojo wa binaadam unakemikali ambazo zimesababisha sumu inayoua viumbe vya ndani ya maji. Msemaji wa wavuvi Manfred Siedler ameliambia gazeti la Bild kuwa waogoleaji wanaojisaidia haja ndogo wanasababisha kemikali aina ya phosphate.

"Tunakadiria kuwa nusu lita ya mkojo inatolewa na kila muogeleaji kwa siku" amekaririwa msemaji huyo. Habari zinasema kutumia dawa za kupambana na phosphate kunagharimu dola laki saba na nusu, na hata hivyo hatua hiyo haijafanikiwa.

Wakazi wa huko wanasema kuna mvutano kati ya wavuvi na waogeleaji katika eneo hilo. Kwa sasa waogeleaji wamepigwa marufuku kufika katika ziwa hilo hadi kemikali hizo zimalizike kabisa.

Polisi wasubiri haja kubwa

Polisi nchini Canada wanasema bado wanamsubiri mtuhumiwa mmoja aliyeiba na kumeza kipande cha almasi, aende haja kubwa ili waweze kupata ushahidi.

Mtandao wa habari wa Stuff.co.nz umesema mtuhumiwa huyo anadaiwa kumeza kipande cha almasi chenye thamani ya dola elfi ishirini wiki iliyopita. Bwana huyo Richard Mackenzie Matthews anadaiwa kuingia katika duka la sonara mjini Ontario na kuiba na kumeza kipande hicho cha almasi.

Mtuhumiwa huyo anashikiliwa na polisi na wapelelezi wamekuwa wakisubiri almasi hiyo yenye uzani wa karati 1.7 itoke kwa njia za asili kutoka tumboni mwake. Sajini wa polisi Brett Corey amesema mtuhumiwa huyo amekwenda chooni mara kadhaa lakini almasi hiyo imegoma kabisa kutoka.

Katika siku za mwanzo mtuhumiwa huyo alikuwa akipewa chakula laini laini, lakini hatua hiyo haikufanikiwa, na hivi sasa bwana huyo anapewa chakula anachotaka yeye. Bado wanasubiri.

Mwili wa zege

Bwana mmoja hapa Uingereza amefanyiwa upasuaji na kisha mwili wake kuzibwa kwa kutumia simenti.

BUILD.....

Bwana huyo, Marek Barden alikuwa na saratani iliyokuwa imeathiri sehemu ya mwili wake yenye uzito wa kilo moja na nusu. Madaktari walitumia saa sita kuondoa eneo lililoathirika pamoja na mbavu sita. Mbali na mbavu hizo bwana huyo pia aliondolewa kishikilio cha pafu la kushoto na sehemu ya kiwambo chake.

Katika kurekebisha, madaktari walilazimika kujenga upya kifua chake kwa kutumia zege. Bwana huyo amesema sasa anajiita mtu wa zege kutokana na mchanganyiko huo. Amesema anahisi tofauti kidogo lakini ameanza kuzoea hali hiyo. Hata hivyo amesema anajiona kuwa ni mtu mwenye bahati sana akikaririwa na gezati la Mirror.

Risasi tena

Mwanamama mmoja nchini Marekani alijipiga risasi mara mbili kabla ya kupiga simu polisi na kudai kuwa amevamiwa na majambazi.

Mwanamama huyo Joy Lounders wa mjini Tennessee alifanya kimbwanga hicho siku ya Ijumaa. Kituo cha habari cha WBIR kimesema mwanamama huyo alijipiga risasi mguuni na kwenye bega ili polisi waamini madai yake hayo.

Wakati akisubiri kupelekwa hospitali kwa kutumia helikopta, mwanamama huyo aliwaambia makachero kuwa kuna mtu aliingia ndani ya nyumba yake na kumshambulia. Amesema alifurumishana na mtu huyo ambaye hatimaye alimpiga risasi mara mbili.

Hata hivyo mazingira ya eneo la tukio yaliwapa wasiwasi polisi. Taarifa zinasema mwanamama huyo alikuwa akitakiwa kuripoto polisi ziku ya Jumatatu kwa kosa la kuendesha gari huku akiwa amelewa, na inawezekana huenda alijipiga risasi ili apate kisingizio cha kutokwenda polisi. Kiomgozi wa polisi wa eneo hilo amesema hana uhakika kama watamfungulia mashtaka mapya ya kujipiga risasi.

Na kwa taarifa yako....... Chakula huchukua takriban sekunde saba kutoka mdomoni hadi kufika tumboni.

-----------------------------

Tukutane Wiki ijayo....... Panapo Majaaliwa....

-----------------------------