Huwezi kusikiliza tena

Bendi ya Bana OK yatoweka DRC

Ndombe Opetum alikuwa mwimbaji mkuu wa Afrisa International, kabla ya kujiunga na bendi ya TPOK Jazz, miaka ya sabini , baada ya Sam Mangwana kuondoka kwenye bendi hiyo.

Alijiunga na OKJazz na mwenzake Empopo Loway na alisalia kwenye bendi hiyo hadi ilipotawanyika mwezi Disemba mwaka1993, miaka minee baada ya mwasisi wa bendi hiyo Luambo Luanzo Makiadi, maarufu kama Franco.

Waimbaji wengine wa bendi hiyo wakati huo walikuwa Wuta Mayi, Michel Boyibanda, Josky Kiambukuta and Youlou Mabiala, na mcheza gita Simaro Lutumba pamoja na Franco mwenyewe. Lubunga Byaombe anasimulia safari ya Ndombe na kuangalia umaarugu wake nchini DRC kabla ya kuaga na kuzikwa siku ya Jumapili mjini Kinshasa.

Bendi hii ya TP OK Jazz ni bendi iliyokua na historia ndefu kuanzia miaka ya 1950. Na kati ya mwaka 1950 na 1960 wanamuziki walioanza bendi wakati huo na kujulikana kama OK Jazz walikua Vicky Longomba, Jean Serge Essous, Fran├žois Luambo Makiadi, De La Lune, Augustin Moniania Roitelet, La Monta LiBerlin, Saturnin Pandi, Nicolas Bosuma Bakili Dessoinand na muimbaji Philippe Lando Rossignol.

Walianza kupiga muziki wao mahali palipojulikana kama Longisa Studios mjini Kinshasa wakiwa wasanii huru wa kujitegemea kabla ya kuunda bendi hii mwaka 1956. Jina OK Jazz lilitokana na klabu cha pombe walipokua wakichezea muziki wao, OKBar. Bendi hii mpya ilikua ikitumbuiza mara kwa mara kwenye Studio ya mjini na mwishoni mwa wiki wakicheza kwenye harusi.

Mwaka 1957,muimbaji kiongozi Philippe Lando Rossignol akaondoka kwenye bendi hiyo na badala yake Edo Nganga kutoka Congo Brazaville akawa muimbaji kiongozi. Baadaye mwaka huo Isaac Musekiwa kutoka Zimbabwe mcheza Saxophone akajiunga na bendi ambayo uongozi wake wakati huo ulikua kati ya Vicky Longomba, Essous na Franco.

Bendi hii ilivunjika baada ya Vicky Longomba na Jean Essous kujiondoa na kumuacha Franco peke yake. Hapa aliamua kuleta waimbaji wapya na kuimarisha bendi. Baadaye Vicky Longomba alipoamua kurudi pamoja na halaiki ya waimbaji wazuri wengi, akiwemo Verckys Kiamungana Mateta na kuanza kukabiliana na Bendi maarufu kipindi hicho ya African Jazz ya Joseph Kabasele, Franco akijivunia miamba ya wanamuziki na kuvutia wanachama wengi Bendi ikapewa jina TP OK Jazz TP ikimaanisha Tout Pouissas.

Miaka ya 1990 - 1993 Bendi hii ilikabilia na kipindi kigumu kufuatia kifo cha kiongozi wake Franco. Ilipata viongozi wapya Simaro Lutumba, Josky Kiambukuta, Ndombe Opetum na Madilu System waliokubaliana na familia ya marehemu Franco kugawana mapato kwa wanamuziki wapokee asili mia 70 na familia ichukuwe asili mia 30. Mpango huu uliendelea kuanzia Agosti mwaka 1989 hadi Disemba 1993.

Kisha mnamo mwezi Disemba mwaka 1993 mipango yote ikavunjika. Familia ya Franco haikutosheka na asili mia 30 kama ilivyokubaliwa, ikitaka pesa zaidi. Hawakuweza kuafikiana na wanamuziki. Hivyo wanamuziki akiwemo marehemo Ndombe Opetum waliamua kurejesha vyombo vya muziki na kuwakabidhi familia ya Franco haki yao na kuunda bendi mpya Bana OK.

Hivyo mwisho wa mojapo ya Bendi kubwa barani Afrika ukafikia kikomo baada ya miaka 37 tangu mwezi Juni 1956 hadi Disemba mwaka 1993.