Ezekiel Kemboi: Nitarudi kutetea medali London

Ezekiel Kemboi Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Kemboi alimaliza wa tatu Rio lakini akapokonywa medali

Mkenya Ezekiel Kemboi, ambaye alikuwa ametangaza kustaafu kutoka kwenye riadha, amedokeza kwamba amebadilisha msimamo wake.

Bw Kemboi, mshindi mara mbili wa mbio za mita 3000 kuruka viunzi na maji Olimpiki, alikuwa ametangaza uamuzi wake wa kustaafu baada ya kumaliza wa tatu katika Olimpiki mjini Rio.

Lakini muda mfupi baadaye, alipokonywa medali hiyo baada ya majaji kuamua kwamba alikiuka kanuni za mbio hizo kwa kukanyaga nje ya mstari.

Mfaransa Mahiedine Mekhissi, aliyemaliza nafasi ya nne, alipandishwa hadi nafasi ya tatu na kupewa nishani ya shaba.

"Nilikuwa nimeamua kustaafu baada ya michezo ya Olimpiki iwapo ningeenda nyumbani na nishani …. Sasa nahisi kwamba ni lazima nirejeshe medali hii si kwa kulalamika lakini kwa kuipigania uwanjani," ameandika kwenye Facebook.

"Kemboi hajastaafu. Nitarejea London 2017 kutetea medali yangu kutoka kwa Ufaransa."

Jiji la London, lililokuwa mwenyeji wa Olimpiki 2012, litaandaa mashindano ya ubingwa wa riadha duniani ya IAAF mwaka ujao.

Kemboi, 34, ndiye aliyeshinda Olimpiki za London 2012 katika michezo ambayo Mfaransa Mahiedine Mekhissi-Benabbad alishinda fedha.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Kemboi alitwaa dhahabu Michezo ya Olimpiki ya London 2012

Mshindi wa mbio za Rio alikuwa Mkenya Conseslus Kipruto ambaye pia aliweka rekodi mpya ya Olimpiki , muda wake ukiwa 8:03.28.

Mmarekani Evan Jager alimaliza wa pili muda wake ukiwa 8:04.28.

Muda wa Kemboi ulikuwa 8:08.47 na wa Mekhissi 8:11.52.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii