Messi kukosa mechi dhidi ya Uruguay

Messi apata jereha Haki miliki ya picha AFP
Image caption Messi apata jereha

Kambi ya Argentina imethibitisha kuwa Messi, mwenye miaka 29, anasumbuliwa na maumivu ya misuli ya pajani ambayo aliyapata Jumapili iliyopita wakati klabu yake FC Barcelona iliifunga Athletic Bilbao 1-0 kwenye La Liga huko Uhispania.

Hadi sasa haijajulikana iwapo Messi atacheza mechi zao mbili za kufuzu kombe la Dunia za Ijumaa dhidi ya Uruguay itakayochezwa huko Mendoza, Argentina na ile inayofuatia ya ugenini huko Merida dhidi ya Venezuela siku 5 baadae.

Messi alijiuzulu kuichezea Argentina mwezi Juni baada ya kushindwa fainali ya Copa America walipobwagwa na Chile lakini baada ya kocha mpya Edgardo Bauza kuteuliwa nahodha huyo wa nchi yake aligeuza uamuzi wake.

Mechi hizo za Argentina zitakuwa chini ya kocha wao mpya Edgardo Bauza kwa mara ya kwanza ambazo pia atawakosa washambuliaji wa Man City Sergio Aguero na kiungo wa Paris St Germain Javier Pastore kwani wote wamejiondoa kikosini kutokana na kuumia.

Nao, Vigogo wengine wa Marekani ya Kusini, Brazil, chini ya kocha mpya Tite, na ambao wako nafasi ya 6 wakiwa na pointi 9 wanakabiliwa na mechi 2 dhidi ya Ecuador na Colombia.

Lakini, wakiongozwa na Neymar, ambae majuzi aliipa Brazil ubingwa wa kwanza wa Olimpiki, wana matumaini makubwa.