Tottenham yamwinda Isco wa Real Madrid

Isco
Image caption Isco

Klabu ya Tottenham Hotspurs inadaiwa kuwa tayari kuvunja rekodi yao kwa kutoa kitita cha paundi milioni 40 kwa ajili ya kumsajili Isco kutoka Real Madrid Januari mwakani.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 24 amekuwa akihangaika kupata nafasi katika kikosi cha Zinedine Zidane, akianza katika mechi mbili pekee msimu huu na alikuwa akihusishwa na tetesi za kwenda Spurs kipindi cha kiangazi.

Madrid wanadaiwa kuwa tayari kumuuza, huku chaguo la kumnasa kwa mkopo na nafasi ya kumnunua moja kwa moja pia ikiwepo.

Isco aliyenunuliwa na Madrid kutoka Malaga miaka mitatu iliyopita tayari ameeleza nia yake ya kuondoka kama atakosa nafasi katika kikosi cha kwanza.

Taarifa kutoka nchini Uhispania zimeripoti kuwa Gareth Bale amekubali kusaini mkataba mpya wa miaka sita na Real Madrid na mabingwa hao wa Ulaya pia wanajipanga kutangaza mikataba mipya ya Cristiano Ronaldo, Pepe na Luka Modric.

Taarifa hizo zinadai kuwa Bale ambaye alijiunga na Madrid kwa ada iliyovunja rekodi ya euro milioni 100 mwaka 2013, anatarajiwa kusaini mkataba mpya ambao utamalizika mwaka 2022 katika kipindi cha wiki mbili zijazo.

Beki wa kati Pepe ambaye mkataba wake wa sasa unamalizika mwakani, naye ataongezewa mkataba mwingine utakaokwisha mwaka 2018.

Ronaldo ambaye ni mfungaji wa wakati wote wa klabu hiyo,anatarajiwa kupewa mkataba utakaomalizika mwaka 2020 sambamba na kiungo mchezeshaji Modric.