EPL: Chelsea walaza Leicester Stamford Bridge

Victor Moses alifungia Chelsea bao la tatu Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Victor Moses alifungia Chelsea bao la tatu

Chelsea wamepokeza mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya England Leicester kipigo cha nne mtawalia ugenini baada ya kuwalaza 3-0 uwanjani Stamford Bridge.

Chelsea walienda kifua mbele dakika ya saba baada ya Nemanja Matic kupindua mpira wa kona uliopigwa na Eden Hazard na Diego Costa akautumbukiza kimiani.

David Luiz alipiga frikiki safi ambalo iligonga mlingoti wa goli kabla ya Pedro kumpa pasi Hazard, ambaye alimpiga chenga Kasper Schmeichel na kufunga dakika ya 33.

Luiz naye alinusurika kujifunga baada ya mpira wake kugonga mlingoti wa goli kipindi cha pili kabla ya Victor Moses kufunga baada ya kupokea pasi kutoka kwa nguvu mpya Nathaniel Chalobah dakika ya 80.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Hazard alifunga bao la pili

Leicester, ambao walimuweka Riyad Mahrez benchi kwa mara ya kwanza wakianza mechi katika mechi 36, hawakuandikisha kombora hata moja la kulenga goli na walionekana kutatizwa na mashambulio ya Chelsea.

Leicester wameshinda mechi mbili pekee kati ya nane walizocheza msimu huu.

Kwa Chelsea, ulikuwa ushindi wao wa nne chini ya meneja mpya Antonio Conte.