Mpango wa kuchezea Uefa Marekani

Cristiano Ronaldo Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Real Madrid walilaza Atletico Madrid kwenye fainali Mei mwaka huu

Rais wa shirikisho la soka la Ulaya (Uefa) amesema bado anafuatilia pendekezo lake la kutaka fainali ya Kombe la Klabu Bingwa Ulaya ichezewe nje ya bara Ulaya.

Aleksander Ceferin, kutoka Slovenia, amesema atafufua tena juhudi zake za kutaka miji iwe ikituma maombi ya kuwa mwenyeji wa fainali hizo.

Amesema anaunga mkono fainali kuchezewa New York.

"Linaweza kuwa wazo tu lakini ni sharti tulizungumzie," amesema Ceferin, ambaye aliteuliwa kuwa mkuu wa Uefa mwezi jana.

Fainali zote 61 zilizochezwa awali zilichezewa Ulaya, lakini Ceferin amesema haliwezi likawa tatizo kwa mashabiki wa soka kusafiri Marekani.

Aliongeza: "Kusafiri kutoka Ureno hadi Azerbaijan kwa mfano ni karibu sawa au ni sawa na kwenda New York."

"Hii ni michuano ya Ulaya kwa hivyo hebu tulifikirie hili."

Kunaweza kuwa na tatizo la nyakati hata hivyo, ikizingatiwa mabadiliko ya saa katika mabara mbalimbali.

Mkuu huyo wa Uefa hata hivyo hana mipango ya kubadilisha wakati wa kuanza kwa fainali, ambayo kawaida huchezwa saa 19:45 BST (20:45 GM).

Fainali zimekuwa zikichezwa Jumamosi tangu 2010.

"Ukiangalia kifedha, hilo haliwezi kufaa. Lakini lazima tufikirie kuhusu masoko mengine pia. China inavutia kama soko, na Marekani pia. Soka inaanza kupata umaarufu huko pia," anasema.