Jurgen Klinsmann atimuliwa kuinoa Marekani

Klinsmann aliifikisha Marekani hatua ya 16 katika kombe la dunia 2014 nchini Brazil
Image caption Klinsmann aliifikisha Marekani hatua ya 16 katika kombe la dunia 2014 nchini Brazil

Mchezaji wa zamani na meneja wa Ujerumani Jurgen Klinsmann ametimuliwa katika nafasi ya ukocha wa timu ya taifa ya Marekani.

Klinsmann mwenye miaka 52 aliyeshinda kombe la dunia akiwa mchezaji mwaka 1990 alianza kukinoa kikosi cha Marekani mwaka 2011.

''Tunaendelea kuwa imara, tuna wachezaji wa kiwango cha juu wa kutusaidia kufuzu kombe la dunia mwaka 2018 nchini Urusi,'' amesema Rais wa shirikisho la soka nchini Marekani Sunil Gulati.

Klinsmann aliifikisha Marekani hatua ya 16 katika kombe la dunia 2014 nchini Brazil.

Sambamba na hilo walipoteza kwa magoli 2-1 wakiwa nyumbani dhidi ya Mexico na baadae kufungwa 4-0 na Costa Rica katika hatua ya kufuzu kombe la dunia.

Marekani inabakia mkiani mwa timu sita ikiwa haina alama yoyote.

Klinsmann mshambuliaji wa zamani wa Tottenham alihusishwa kuinoa timu ya taifa ya England baada ya Sam Allardyce kubwaga manyanga mwezi Septemba.