Kenya ya kwanza kuaga mashindano Cameroon baada ya kulazwa 3-1

Kenya walichapwa 3-1 na Mali na Ghana Haki miliki ya picha CAF / TWITTER
Image caption Kenya walichapwa 3-1 na Mali na Ghana

Kina dada wa Kenya wamekuwa timu ya kwanza kuaga mashindano ya taifa bingwa Afrika upande wa wanawake baada ya kulazwa 3-1 na Mali.

Hiyo ilikuwa mara ya pili kwa Harambee Starlets, ambao walikuwa wanacheza fainali hizo mara ya kwanza, kushindwa katika mashindano hayo.

Mechi ya kwanza walilazwa 3-1 na Ghana.

Mali walijikwamua kutoka kichapo cha 6-0 mikononi mwa Nigeria mechi yao ya kwanza na kujiimarishia matumaini ya kufuzu kwa nusu fainali.

Ushindi dhidi ya Ghana katika mechi ya mwisho Kundi B Jumamosi mjini Yaounde utawahakikishia nafasi za kufuzu hadi hatua ya nne bora.

Bassira Toure alifungia Mali mabao mawili kipindi cha pili baada ya Sebe Coulibaly kufungua ukurasa wa mabao kupitia mkwaju wa ikabu kipindi cha kwanza dhidi ya Kenya.

Cheris Avilia alifungia Kenya bao la kufutia machozi dakika za mwisho mwisho.

Kenya, waliokuwa wameonyesha mchezo mzuri dhidi ya Ghana hawakuweza kucheza vyema dhidi ya Mali ambao walionekana kujiamini sana licha ya kupokezwa kipigo kizito na Nigeria mechi yao ya kwanza.

Starlets watacheza mechi yao ya mwisho dhidi ya mabingwa watetezi Nigeria Jumamosi.

Mada zinazohusiana