Kompany kuwa nje zaidi ya wiki nne

Kompany Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Vincent Kompany ameshiriki mechi tano msimu huu

Nahodha wa Manchester City Vincent Kompany atasalia nje ya uwanja kati ya wiki nne hadi sita kutokana na jeraha la goti,meneja Pep Guardiola amethibitisha.

Mbeligiji huyo alitolewa uwanjani siku ya Jumamosi walipokuwa wakiminyana dhidi ya Crystal palace.

Manchester City walipata ushindi wa mabao 2-1 katika uwanja wa Selhurst.

Kompany mwenye umri wa miaka 30, amefanyiwa uchunguzi na Dkt Ramon Cugat huko Barcelona, na pia daktari wa timu yake ya Manchester City.

''Dkt Cugat amedhibitisha kile ambacho daktari wa klabu hiyo alichosema. Atakuwa nje ya uwanja kwa wiki nne hadi sita ,'' amesema Guardiola.

Kompany ameshiriki kwa kikosi cha kwanza katika mechi mbili za ligi msimu huu, na amepata jeraha la mguu na paja mwaka 2016.

Changamoto yake ya hivi karibuni, ni jeraha lake la 35 tangu kujiunga kwake na Manchester City kutoka kwa klabu ya Ujerumani ya Hamburg mwaka 2008.