Rooney kuepuka adhabu ya FA

Rooney Haki miliki ya picha Getty Images

Nahodha Wayne Rooney, hataadhibiwa kwa utovu wa nidhamu alipokuwa na timu ya taifa.

Mshambuliaji wa Manchester United, aliomba radhi kwa picha zake 'zisizofaa' alizopigwa akiwa kwenye sherehe ya harusi baada ya ushindi wa England mechi ya kufuzu kwa Kombe la Dunia dhidi ya Scotland.

Gazeti la Daily Mirror limeripoti kwamba Chama cha Soka Uingereza, FA, kilibaini kwamba Rooney alikuwa amealikwa kwenye harusi hiyo na hakujiweka hatarini.

Rooney,31, amehakikishiwa na wakuu kutoka FA kwamba hataadhibiwa.

Uchunguzi ulianzishwa baada ya gazeti la The Sun kuchapisha picha ambazo lilimuonyesha akiwa amelewa kwenye sherehe hiyo ya siku Jumamosi, tarehe 12 Novemba.

FA inachunguza madai kwamba baadhi ya wachezaji wa England walikuwa nje siku hiyo ya Jumamosi usiku baada ya ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Scotland siku tatu kabla ya kutoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Uhispania katika mechi ya kirafiki.

Wachezaji wa England walirudi hoteli saa 11:00 GMT siku ya Jumapili kama walivyohitajika, na kuhudhuria mafunzo ya mchana.

Wachezaji wa England wamepigwa marufuku na shirikisho la FA kwa kukaa nje usiku wakiwa katika majukumu ya kimataifa.