Yannick Bolasie kufanyiwa upasuaji wa goti

Yannick Bolasie Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Yannick Bolasie

Winga wa klabu ya Everton Yannick Bolasie, atafanyiwa upasuaji wa goti baada ya uchunguzi kubaini kwamba alipata jeraha baya kwenye kano za goti walipokuwa wakikabiliana na Manchester United siku ya Jumapili.

Mchezaji huyo raia wa DR Congo alisaini mkataba na Everton kutoka Crystal Palace kwa kitita cha pauni milioni 25 mwezi Agosti.

Bolasie ameshiriki mechi zote msimu huu kwenye klabu ya Everton.

Bolasie, 27, alipata jereha katika mguu wake wa kulia dakika ya 68 ya mchezo siku ya Jumapili walipotoka sare ya 1-1 uwanjani Goodison Park.

Winga huyo atahitajika kujikakamua kurudi uwanjani kabla msimu huu wa ligi ya Premia kukamilika.

Bolasie, alichezea klabu ya Crystal Palace kwa misimu minne baada ya kutoka Bristol City mwaka 2012 kabla ya kuhamia Everton.

Nyota huyo hatashiriki michuano ya Kombela Taifa Bingwa Afrika nchini Gabon mwezi ujao.

Kabla ya jeraha la Bolasie, meneja wa Everton Ronald Koeman, alikuwa amezungumzia suala la kusajili mshambuliaji wa Manchester United Memphis Depay, 22, kwa mkopo ifikapo mwezi Januari.

Mada zinazohusiana