Raia wa Uganda ashinda tuzo ya kocha bora Kenya

Mkufunzi kutoka Uganda Paul Nkata
Image caption Mkufunzi kutoka Uganda Paul Nkata

Washindi wa tuzo za wanasoka bora katika ligi kuu ya soka nchini Kenya walituzwa katika hafla ya kufana iliyoandaliwa mjini Nairobi.

Shughuli hiyo iliwashirikisha makocha, manahodha wa timu mbalimbali na wawakilishi wa waandishi wa habari za spoti.

Kiungo wa klabu ya Western Stima, Kenneth Muguna ambaye anashiriki ligi hiyo kwa msimu wake wa kwanza, ndiye mchezaji bora wa ligi hiyo.

Muguna alimpiku kiungo wa zamani wa Azam anayeichezea Tusker, Humphrey Mieno na kuondoka na mataji mawili, baada ya kutangazwa kuwa mchezaji bora wa ligi na kiungo bora wa mwaka.

Tuzo ya mchezaji mpya wa ligi ilinyakuliwa na Beki machachari wa klabu ya Gor Mahia, Eric 'Marcelo' Ouma.

Mabingwa wa ligi, Tusker waliondoka na tuzo kadhaa baada ya meneja wake, Goerge Opondo kutajwa meneja wa mwaka na Mkufunzi wao, Kocha wa Uganda, Paul Nkata, 'Latest' kukabidhiwa taji la kocha bora na kuwa kocha wa kwanza kutoka nchi jirani kushinda tuzo hiyo.

Nkata aliiwezesha timu yake kuondoka na kombe la ligi kuu na ngao ya Gotv. ''Nafurahi sana kutunukiwa kwani ilikuwa ni msimu mgumu ulio na ushindani mkubwa,'' alsema.

Image caption Kenneth Muguna alishinda tuzo ya mchezaji bora wa ligi hiyo

Nkata alikuwa akiwania tuzo hiyo dhidi ya kocha wa mabingwa mara tatu mfululizo wa ligi hiyo, Ze Maria, na kocha wa klabu ya Posta Rangers, Zedekiah Otieno.

Kwa upande wa marefa, Anthony Ogwayo alituzwa kwa uamuzi wake kwenye ligi na kupokea shilingi laki mbili naye Gilbert Cheruiyot akitajwa kuwa Naibu refa bora wa mwaka.

Washindi zaidi:

Kipa bora wa mwaka - Patrick Matasi - Posta Rangers.

Mfungaji bora - John Makwatta Ulinzi Stars

Beki bora wa Mwaka - Joackins Atudo - Posta Rangers

Mchezaji mwenye nidhamu bora- Ali Bhai - Kakamega Homeboyz

Timu yenye nidhamu bora - Kakamega Homeboyz

Mada zinazohusiana