Chapecoense wapangiwa mechi ya kwanza Brazil

Alan Ruschel Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Alan Ruschel, mmoja wa wachezaji walionusurika ajali ya ndege, alirejea Brazil mnamo Jumanne

Klabu ya Chapecoense itacheza mechi ya kwanza tangu kutokea kwa ajali ya ndege iliyoangamiza wengi wa wachezaji wake tarehe 29 Januari.

Maafisa katika klabu hiyo ya Brazil wameambia BBC kwamba klabu hiyo imepangiwa kucheza dhidi ya International de Lage nyumbani katika mechi ya ligi ya ubingwa wa jimbo.

Ndege iliyobeba wachezaji na maafisa wa timu hiyo iliishiwa na mafuta na kuanguka Medellin, Colombia mnamo 28 Novemba, na kuua watu 71, wakiwemo wachezaji na maafisa wa klabu hiyo.

Wachezaji watatu wa klabu hiyo walikuwa miongoni mwa manusura sita.

Wachezaji tisa hawakusafiri.

Wachezaji wawili kati ya walionusurika, beki Alan Ruschel na kipa Jakson Follmann, ambaye amekatwa mguu wake, walirejea Brazil Jumanne.

Wa tatu, neto, bado amelazwa hospitalini Colombia.

Vagner Mancini ameteuliwa meneja na kupewa jukumu la kuunda upya timu hiyo kutoka mji wa Chapeco, kusini mwa Brazil.

Klabu kubwa Brazil zimeahidi kuikopesha Chapecoense wachezaji bila malipo na pia zikaomba timu hiyo ilindwe dhidi ya kushushwa daraja misimu mitatu ijayo.

Mchezaji wa zamani wa Brazil na Barcelona Ronaldinho na nyota wa zamani wa Argentina Juan Roman Riquelme wanadaiwa kujitolea kuichezea klabu hiyo.

Mchezaji wa zamani wa Barca Eidur Gudjohnsen, pia yuko tayari kuchezea klabu hiyo.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii