Bernard Hopkins apigwa knockout pigano la mwisho

Bondia Bernard Hopkins kulia Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Bondia Bernard Hopkins kulia

Bernard Hopkins alishindwa katika pigano lake la mwisho baada ya bingwa huyo wa ndondi mwenye umri wa miaka 51 kupigwa kwa njia ya knockout katika raundi ya nane na Joe Smith Jr.

Makonde makali aliomiminiwa Hopkins yalimsukuma katika kamba na baada ya kushindwa kurudi ulingoni kwa sekunde 20 mpinzani wake alitangazwa mshindi kwa njia ya knockout.

Hopkins alisema kuwa alisukumwa kabla ya kichwa chake kugonga chini alipoanguka katika pigano hilo la uzani wa Light Heavy.

''Nilijiumiza kifundo changu cha mguu na singeweza kusimama''.

Hopkins amethibitisha kuwa pigano hilo litakuwa lake la mwisho katika kipindi cha miaka 28 katika ndondi, ambapo alimaliza akiwa na ushindi wa mapigano 55, akishindwa mara 8 na kupata sare mara mbili.

Bingwa huyo wa uzani miwili tofauti duniani alitetea taji lake la ukanda wa middleweight mara 20 kati ya mwaka 1995 na 2005 na ndiye bondia mwenye umri mkubwa zaidi kushikilia taji akiwa na umri wa miaka 49.