Chapecoense kuwanunua wachezaji 20 Brazil

Mashabiki wa soka Brazil wamekuwa wakitoa heshima zao kwa wachezaji waliofariki Haki miliki ya picha AFP
Image caption Shabiki wa soka Brazil akitoa heshima zake kwa wachezaji waliofariki

Klabu ya Chapecoense nchini Brazil, ambayo iliwapoteza wachezaji wengi kwenye ajali ya ndege Novemba, imetangaza kwamba itawanunua wachezaji 20 wapya wa kucheza msimu ujao.

Wachezaji walionusurika ajali hiyo hata hivyo watahifadhiwa nambari zao za jezi.

Wachezaji 19 wa klabu hiyo walifariki kwenye ajali ya ndege klabu hiyo ilipokuwa safarini kwenda kucheza fainali ya Copa Sudamericana.

Klabu hiyo baadaye ilitunukiwa kikombe hicho na wapinzani wao kutoka Colombia Atletico Nacional wakapewa tuzo ya uchezaji haki.

"Sasa tunalazimika kutumia mikopo," mkurugenzi wa soka Rui Costa alisema.

Beki wa kati Neto na mkabaji kamili Alan Ruschel walinusurika na Costa amesema wanatarajia wachezaji hao watarejea na kuvalia jezi zao.

Kipa wa akiba Jackson Follmann pia alinusurika lakini amekatwa sehemu ya mguu wake.

Chapecoense watacheza mechi yao ya kwanza 26 Januari kwa mechi ya nyumbani dhidi ya Joinville.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii