Barcelona ''kuamua'' kuhusu kandarasi mpya ya Messi

Mshambuliaji wa Barcelona Lionel Messi Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Mshambuliaji wa Barcelona Lionel Messi

Uwezo wa klabu ya Barcelona kumpatia Lionel Messi kandarasi mpya yenye nyongeza ya mshahara itategemea uwezo wao wa kuvutia mapato kutoka kwa wadhamini na uuzaji wa wachezaji ,amesema mkurugenzi mkuu wa klabu hiyo Oscar Grau.

Kandarasi ya Messi inakamilika 2018 na anatarajia kupewa mkataba mpya huku ikiripotiwa huenda akapewa kitita cha pauni milioni 21 wanazopata Luis Suarez na Neymar.

''Tunahitaji wachezaji wazuri lakini pia lazima kuwa na kipaumbele '',aliongezea.

La Liga huweka mkataba na kila klabu kuhusu matumizi yao kila mwanzo wa msimu, ambapo huyazuia mabodi kutotumia zaidi ya asilimia 70 ya bajeti yake ya mapato.

Kandarasi zenye mishahara mikubwa walizopatiwa Suarez na Neymar ambazo zitakamilika 2021, huchukua kiwango kikubwa cha matumizi ya timu hiyo.

Messi mwenye umri wa miaka 29, anaripotiwa kupokea pauni milioni 19 na Grau anasema kuwa nyongeza yoyote lazima ifikiriwe sana.