Pogba: Mourinho aliniambia nijisikie huru uwanjani

Kiungo wa kati wa Man United Paul Pogba Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Kiungo wa kati wa Man United Paul Pogba

Kiungo wa kati wa Manchester United Paul Pogba anasema kuwa kuimarika kwa mchezo wake hivi karibuni kunatokana na mkufunzi wake Jose Mourinho kumwambia ajisikie ''huru uwanjani''.

Raia huyo wa Ufaransa mwenye umri wa miaka 23 alianza kuichezea klabu hiyo akiwa katika kiwango cha chini cha mchezo wake baada ya kujiunga na Manchester United.

Lakini amechangia pakubwa katika ushindi wa mechi tisa bila kushindwa wa Manchester United.

''Aliniambia nisimsikize mtu yeyote ,nicheze mchezo wangu na kujifurahisha.

Hivyo ndivyo nifanyavyo'', Pogba aliambia BBC.

''Pogba anacheza na motisha akituonyesha kitu anachoweza kufanya''.

Kulikuwa na matumaini makubwa kufuatia kurudi kwa Pogba katika uwanja wa Old Trafford kutoka Juventus mnamo mwezi Agosti, lakini ni kuanzia hivi karibuni ambapo ushawishi wake katika timu hiyo umeanza kuonekana.