AFCON 2017: Kongo yaikaba koo Morocco

Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo imeweka matatizo yake ya malipo pembeni na kuicharaza Morocco kwa 1-0 kwenye mchezo wake wa ufunguzi wa Kombe la mataifa ya Afrika nchini Gabon.

Haki miliki ya picha ISSOUF SANOGO
Image caption Junior Kabananga alifunga bao pekee

Kikosi cha Floribert Ibenge kilichofanya mgomo siku ya Ijumaa kutokana na kutolipwa bakshishi zao, almanusura wafungwe bao la mapema kwenye uwanja wa Stade d'Oyem, baada ya Mbarak Boussoufa kugonga mwamba.

Junior Kabananga, ndiye aliyefunga bao la ushindi katika dakika ya 55.

DRC walimaliza wakiwa mchezaji mmoja pungufu baada ya Lomalisa Mutambala kutolewa nje kwa kuoneshwa kadi mbili za manjano. Mutambala aliingia kama mchezaji wa akiba, na kutolewa baada ya dakika 16.

Youssef El-Arabi wa Morocco alishindwa kufunga katika nafasi mbili alizopata kwa kichwa, mwishoni mwa mchezo.

DRC walilazimika kucheza wakiwa tisa tu uwanjani kwa muda baada ya Mutambala kutolewa na beki Gabriel Zakuani kuumia na kutoka nje.

Kongo Kinshasa sasa inaongoza Kundi C baada ya mchezo wa awali kati ya mabingwa watetezi Ivory Coast kutoka sare ya 0-0 na Togo.