Yaya Toure akataa £430,000 kwa wiki kutoka China

Yaya Toure na Kocha Pep Guardiola
Image caption Yaya Toure na Kocha Pep Guardiola

Kiungo wa kati wa klabu ya Manchester City Yaya Toure amekataa ombi la mshahara wa pauni 430,000 kwa wiki kutoka China.

Toure mwenye umri wa miaka 33 amevutia timu nyingi katika ligi ya China ,wakati ilipoonekana kwamba huenda asishirikishwe katika mechi zozote chini ya mkufunzi Pep Guardiola.

Aliamua kutoondoka wakati huo na akakataa tena alipopewa kitita hicho wakati wa dirisha hili la uhamisho.

Kandarasi ya raia huyo wa Ivory Coast inakamilika msimu huu.

Amekuwa mchezaji muhimu wa City tangu aliporudishwa katika kikosi cha kwanza na alianza mechi yake ya saba mfululizo wakati wa kushindwa kwa 0-4 dhidi ya Everton katika mechi ya ligi ya Uingereza hapo Januari 15.

Toure amekuwa huru kuingia katika kanadarasi na vilabu vingi ughaibuni tangu mwezi Januari lakini imedaiwa kwamba bado anapenda ligi ya Uingereza.

Toure hajapata hakikisho lolote kuhusu kandarasi kutoka kwa kocha wake Guardiola.