Gabriel Jesus ahamia rasmi Man City

Gabriel Jesus Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Gabriel Jesus amefungia Brazil mabao manne katika mechi sita alizowachezea

Klabu ya Manchester City imepata idhini ya kumnunua rasmi winga wa Brazil wa umri wa miaka 19 Gabriel Jesus na sasa anaweza akacheza dhidi ya Tottenham Jumamosi.

Jesus amehamia City kutoka klabu ya Palmeiras ya Brazil kwa £27m.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Brazil alikubali kuhamia City kwa mkataba wa miaka mitano Agosti mwaka jana.

Alisalia na Palmeiras hadi mwisho wa msimu wa soka Brazill mwezi Desemba.

"Ana uwezo wa kuibuka kuwa miongoni mwa washambuliaji bora zaidi katika soka," mkurugenzi wa soka wa City Txiki Begiristain alisema.

Jesus alifika City mwanzoni mwa mwezi huu lakini alichelewa kupata idhini ya kusajili wa City, taarifa zikisema Shirikisho la Soka la Uingereza lilikuwa linachunguza stakabadhi kuhusu uhamisho wake.

City wanamchukulia mchezaji huyo kuwa chipukizi mwenye kipaji zaidi Amerika Kusini kwa sasa, na waliwapiku Barcelona kumchukua.

Jesus amesema meneja wa City Pep Guardiola alichangia sana katika uamuzi wake wa kuhamia klabu hiyo.

City kwa sasa wamo nambari tano kwenye jedwali Ligi ya Premia, alama 10 nyuma ya viongozi Chelsea baada ya kulazwa mechi mbili kati ya tatu walizocheza karibuni zaidi.

Mbona anaitwa Jesus?

Jesus alikuwa awali akifahamika kama Gabriel Fernando alipoanza kuchezea kikosi cha kwanza Palmeiras akiwa na miaka 17.

Taarifa ya City imesema: "Akifahamika wakati huo kama Gabriel Fernando, alipewa jezi nambari 33 - umri wa Kristo - na afisa mmoja wa habari wa Palmeiras alimshawishi kubadili jina na kuwa Gabriel Jesus.

"Alichezeshwa katika timu kuu ya Palmeiras mara ya kwanza na Oswaldo de Oliveira mnamo 7 Machi 2015, alipoingia dakika ya 73 mechi ambayo walishinda 1-0 dhidi ya CA Bragantino katika uwanja wa Allianz Parque."

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii