Wakuu wa soka wa Saudi Arabia waomba radhi waathiriwa wa shambulio Uingereza

Timu ya Australia Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Timu ya Saudi haikuungana na Timu ya Australia kwa kushikana mikono.

Wakuu wa chama cha soka cha Saudi Arabia wameomba msamaha baada ya timu ya taifa hilo kutoshiriki katika kukaa kimya dakika moja kwa heshima waathiriwa wa shambulio la London Bridge.

Wachezaji wa Australia walishikanisha mikono yao kama ishara ya heshima kabla mechi hiyo ya siku ya Alhamisi ya kufuzu kwa Kombe la Dunia iliyochezewa katika uwanja wa Adelaide Oval uliopo kaskazini mwa Australia.

Wachezaji wa Saudi walionekana kujishughulisha zaidi na kujipangia nafasi uwanjani.

Mbunge mmoja wa Australia ametaja kisa hicho kama ''cha aibu''.

Viongozi wa soka wamesema walikuwa wamearifiwa hapo awali kwamba mila na ''tamaduni za Australia hazikuwa zinaambatana na mila za Wasaudia.''

Chama cha soka cha Saudi Arabia kiliomba radhi siku ya Ijumaa.

''Wachezaji hao hawakuwa na madhumini ya kutoheshimu makumbusho ya waathiriwa ama kusababisha ghadhabu kwa familia zao, marafiki au mtu yeyote aliyeathirika na mkasa huo,'' walisema katika taarifa.

''Chama cha soka cha Saudi Arabia kinalaani vitendo vyote vya kigaidi na kutoa salamu zao za rambirambi kwa familia za waathiriwa, serikali na watu wote wa Uingereza.''

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Uamuzi huo ulishtumiwa nchini Australia

Kimya cha dakika moja kilikuwa kimepangwa na shirikisho la soka la Australia (FFA), waliosema walikuwa wamearifiwa hapo awali kwamba wachezaji wa Saudia ''wangeheshimu mila zetu wakiwa uwanjani.''

Wanasiasa kadhaa wa Australia waliishtumu timu ya Saudia.

''Hili halihusiani na mila," mbunge mmoja , Anthony Albanese alikiambia kituo cha televisheni cha Nine nchini humo.

''Huu ni ukosefu wa heshima na nilifikiri ni jambo la aibu.''

Raia wawili wa Australia , Kirsty Boden na Sara Zelenak walikuwa miongoni mwa watu wanane waliofariki katika mashambulio hayo.

Mada zinazohusiana