Crystal Palace yailaza Chelsea 2-1

Wlifried Zaha akifunga bao lake la pili na la Ushindi dhidi ya Chelsea Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Wlifried Zaha akifunga bao lake la pili na la Ushindi dhidi ya Chelsea

Wilfried Zaha alifunga bao la ushindi huku Crystal Palace ikiandikisha ushindi wake wa kwanza dhidi ya mabingwa wa ligi ya Uingereza Chelsea.

Palace ilikuwa imepoteza mechi zake zote saba tangu ligi ianze zikiwemo mechi tatu chini ya Mkufunzi mpya Hodgson na walikuwa wameshindwa kufunga hata bao moja.

Lakini walimaliza tatizo hilo la kutofunga bao baada ya Yohan Cabaye kusababisha bao ambalo lilimgonga beki wa Chelsea David Luiz na kuingia.

Lakini uongozi huo wa Palace ulisimama kwa dakika nane pekee baada ya kona iliopigwa na Fabregas kufungwa na Tiemoue Bakayoko.

Lakini Zaha, akiwa amerudi baada ya kuuguza jeraha aliweza kufunga bao la pili kabla ya kukamilika kwa kipindi cha kwanza na kikosi hicho cha Hodgson kikaweza kuzuia ushindi huo hadi kipenga cha mwisho.

Ushindi huo hatahivyo hautaiondoa Palace katika mkia wa jedwali lakini umepunguza pengo hilo hadi pointi nne.

Chelsea nao watasalia katika nafasi ya nne wakiwa sasa wako na alama tisa nyuma ya viongozi wa ligi Manchester City.

Mada zinazohusiana