Historia ya London Marathon

Martin Lel, mmoja wa wanariadha kutoka Kenya walioshinda mbio za London Marathon.
Image caption Martin Lel, mmoja wa wanariadha kutoka Kenya walioshinda mbio za London Marathon.

Kila mwaka, jiji la London hupata msisimko wa kipekee kutokana na vishindo vya mbio za London Marathon. Wanariadha maarufu kutoka sehemu mbalimbali duniani, watu maarufu na wananchi wengine wataanza mbio hizo eneo la Greenwich Park kusini mashariki ya London na kukatiza mitaa mbalimbali kisha kumaliza mbio hizo katika eneo la The Mall.

Kuanzishwa kwa mbio hizi za marathon mwaka 1981 kulilenga kuhamasisha watu kukimbia mbio ndefu, kuchangisha fedha kwa ajili ya mambo mbalimbali yenye umuhimu kijamii na kuwajengea wananchi hali ya umoja.

Mwaka huu ni wa 29 na inakisiwa kiasi cha pound milioni 450 zimekusanywa kwa ajili ya hisani mbalimbali. Mbio hizi zinashikilia rekodi katika kitabu cha Guiness kama tukio kubwa kuweza kuchangisha fedha nyingi zaidi kwa mwaka.

Tukio hili huvuta watazamaji wengi katika mitaa na baa nyingi hugeuka kuwa vituo vya ushangiliaji kwa wakimbiaji hao wa hisani. Pengine huenda wakimbiaji kadiri wanavyopita katika mitaa huleta hamasa kwa washangiliaji nao kukumbuka viatu vyao vya mazoezi. Lakini pia jambo jingine muhimu ni kukumbuka namna wazo la mbio hizi lilivyoibuka kwa mara ya kwanza usiku mmoja ndani ya baa katika eneo la Richmond Park.

Hamasa

Chris Brasher hakuwa mgeni katika mambo ya riadha. Kwani mwaka 1954 alikuwa miongoni mwa wakimbiaji (wanaoweka viwango vya kasi) waliomsaidia Roger Bannister kuwa mtu wa kwanza kukimbia maili moja chini wa muda wa dakika nne. Akashinda pia medali ya dhahabu katika mbio za mita 3,000 (steeplechase) katika mbio za Olympics za Melbourne mwaka 1956.

Basher hakuwa na haja yoyote na mbio za marathon, lakini alijenga shauku hiyo baada ya usiku mmoja kutembelea Dysart Arms katika eneo la Richmond na kufanya maongezi juu ya mbio za marathon. Hatimaye akaamua kushiriki katika mbio maarufu za marathoni za New York mwaka 1979.

Basher aliporudi Uingereza baada ya mbio hizo, alikuwa na nia ya kuona kama kuna uwezekano London inaweza kuandaa tukio kama hilo ili kuwaunganisha watu mbalimbali.

Akishirikiana na rafiki yake aitwaye John Disley, Brasher akaweza kupata udhamini wa mbio hizo na baraka kutoka halmashauri ya jiji la London, polisi na vyama vya riadha ili kufanikisha azma yake.

Tarehe 29 mwezi wa tatu 1981, maelfu ya watu walikusanyika katika bustani ya Greenwich, na ilipotimu saa tatu asubuhi mbio za maili 26.2 zikaanza.

Masaa mawili, dakika 11 na sekunde 48 baadaye, wakimbiaji Dick Beardsley na Inge Simonsen wakawa wa kwanza kukatiza mstari wa mwisho katika eneo la Constitution Hill, nyuma ya Buckingham Place na kumaliza mbio za marathoni za London.

Mabadiliko

Tukio hili limezidi kukua na kupata umaarufu toka mbio za kwanza miaka 28 iliyopita. Mwaka 1981, wakimbiaji 20,000 waliomba kushiriki. Ilipofika 2008, idadi iliongezeka na kufika 92,000.

Waratibu wa mbio hizi wamelazimika kubadili mara kadhaa njia za mbio hizi ili kuendana na mabadiliko katika mwonekano wa jiji la London. Wakati eneo la Canary Wharf lilipokuwa likifanyiwa mabadiliko makubwa miaka ya 1980 na 1990, waratibu walilazimika kutafuta njia mbadala katika maeneo mengi yaliyokuwa na shughuli za ujenzi.

Japokuwa eneo la kuanza mbio hizi limeendelea kuwa lile lile, kumekuwa na mabadiliko ya eneo la kumaliza. Mwaka 1983, mstari wa kumaliza mbio ulihamishwa kutoka Constitution Hill kwenda daraja la Westminster. Ukadumu hapo hadi 1993. Wakati wa ukarabati wa daraja mwaka 1994, waratibu wa mbio wakateua The Mall kuwa eneo jipya la kukamilisha mbio za marathoni za London.

Siku za usoni

Chris Basher, mtu aliyewezesha kuleta mbio za marathoni jijini London alifariki mwaka 2003. Lakini miaka saba baada ya kifo chake, mbio hizi bado ziko imara.

Mwaka huu, kampuni ya Virgin ndiyo mdhamini mkuu wa mbio hizi badala ya kampuni ya Flora iliyofanya hivyo kwa miaka mingi. Kampuni ya Virgin imetangaza kuwa kuna matumaini wakimbiaji wataweza kukusanya kiasi cha pauni milioni 250 katika miaka mitano ya udhamini wake.

Sir Richard Branson, mwenyekiti wa makampuni ya Virgin anasema, “Ni tukio la kishujaa na kutia moyo na fedha nyingi zinazokusanywa ni kwa ajili ya mambo ya hisani kwa jamii. Ni tukio moja kubwa kabisa la kuchangisha fedha duniani katika siku moja na tungependa lizidi kukua”