Nigeria yasuasua kujiandaa kwa Afrika Kusini

Mchezaji wa timu ya taifa ya Nigeria.
Image caption Nigeria imekuwa na matatizo kadhaa yanayotishia ufanisi mzuri katika Kombe la Dunia nchini Afrika Kusini.

Waziri wa michezo wa Nigeria ameelezea kutofurahishwa na sehemu itakapokaa timu ya taifa ya nchi hiyo wakati wa mashindano ya Kombe la Dunia nchini Afrika Kusini mwezi Juni.

Super Eagles walikuwa wamepangiwa kukaa kwenye hoteli ijulikanayo kama Hampshire nje kidogo ya jiji la Durban kwa kipindi chote cha mashindano.

Mpango huo sasa uko mashakani baada ya Waziri, Ibrahim Bio, alisema hoteli hiyo haina hadhi inayostahili.

"Nina wasi wasi kuhusu kelele [na] sina uhakika kuhusu usalama katika eneo hili," alisema.

Waziri huyo aliongeza: "Utakabaliana kwamba ni muhimu vijana wetu kuwa katika mazingira salama."

Msemaji wa hoteli hiyo alieleza BBC kuwa hawezi kuzungumzia swala hilo, akiongeza kuwa Fifa wanalishughulikia.

Maandalizi ya Nigeria kwa ajili ya Kombe la Dunia imevurugika kutokana na matatizo mbali mbali - ikiwa ni pamoja na kufutwa kwa kambi ya mazoezi mjini London.

Matumaini

Lakini Shirikisho la Soka la Nigeria (NFF) limesema ufumbuzi utapatikana.

"Siku zote tumekuwa na mpango wa akiba endapo hoteli ingeshindwa kukidhi matakwa yetu na matarajio," msemaji wa NFF, Ademola Olajire aliieleza BBC siku ya Alhamisi.

"Ujumbe unaozuru Afrika Kusini unatarajiwa kurejea karibuni na utawasilisha ripoti kwa umma kwa muda unaostahili.

"Si hali nzuri kuwa nayo, lakini tutafanya mabadiliko muhimu haraka iwezekanavyo."

Katika kundi B kwenye michuano ya Kombe la Dunia, Nigeria watacheza na Argentina, Ugiriki na Korea Kusini.