Tottenham yapaa nafasi ya nne

Shuti kali lililopigwa na kiungo Tom Huddlestone limeweza kuipatia nafasi Tottenham ushindi muhimu dhidi ya Bolton na kuisogeza karibu kabisa kumalizia katika nafasi nne za msimamo wa Ligi Kuu ya England.

Image caption Wachezaji wa Tottenham wakishangilia bao

Kwa matokeo hayo Tottenham imejizatiti katika nafasi ya nne ikiwa na jumla ya pointi 67.

Lakini pamoja na ushindi huo Bolton walikufa kiume na ilikuwa ustadi wa mlinda mlango wa Tottenham, Heurelho Gomes aliyefanya kazi ya ziada kuokoa mashuti ya Matthew Taylor.

Nayo Manchester City imefanikiwa kurejesha matumaini ya kumaliza katika nafasi nne bora baada ya kuilaza mabao 3-1 Aston Villa waliokuwa nao wanawania nafasi hiyo.

Walikuwa ni Villa walioonesha ari ya ushindi kwa kuanza kufunga bao lililowekwa wavuni na John Carew.

Image caption Mshambuliaji wa Manchester City Adebayor akishangilia bao

Carlos Tevez alisawazisha kwa mkwaju wa penalti baada ya Stephen Warnock kumuangusha Adam Johnson ndani ya sanduku la hatari kabla ya Emmanuel Adebayor kupachika bao la pili kwa shuti la karibu.

Craig Bellamy aliihakikishia pointi tatu muhimu Manchester City kwa kupachika bao la tatu baada ya kazi nzuri ya Shaun Wright Phillips kuipangua ngome ya Villa katika dakika za mwisho za mchezo.

Matokeo mengine Birmingham iliilaza Burnley iliyoshuka daraja mabao 2-1, huku wanyonge wa Ligi hiyo walioshuka daraja mapema Portsmouth ilizinduka usingizini na kuwalaza Wolves mabao 3-1 na Stoke City walilazimishwa kwenda sare bila kufungana na Everton.