Neil Robertson bingwa wa Snooker duniani

Neil Robertson ametwaa taji la ubingwa wa dunia kwa mchezo wa snooker baada ya kumshinda Graeme Dott 18-13 na kuwa Muaustralia wa kwanza kushinda ubingwa wa dunia kwa mchezo huo.

Image caption Neil Robertson akishangilia ubingwa

Robertson, ambaye kwa ushindi huo amepanda na kufikia mchezaji bora nambari mbili duniani, awali alikuwa nyuma kwa pointi 5-3 lakini akaweza kujikwamua na kuanza kuongoza licha ya kuonekana baadhi ya nyakati akitetereka.

Anakuwa mchezaji wa kwanza kutoka nje ya Uingereza na Ireland kushinda ubingwa wa dunia tangu Mcanada Cliff Thorburn aliposhinda taji hilo mwaka 1980.

Hata hivyo umaarufu wa mchezo wa snooker uliingia dosari baada ya kufungiwa kucheza bingwa wa dunia kwa mwaka 2009 John Higgins kufuatia tuhuma za rushwa.

Sherehe

Nyumbani kwao Robertson mjini Melbourne kumeandaliwa sherehe kubwa wakati raia wa nchi hiyo walipokuwa wakifuatilia kijana wao akiweka historia ya kuwa Muastralia wa kwanza kunyakua ubingwa wa dunia kwa mchezo wa snooker.

Muda mfupi baada ya kutumbukiza mpira wa mwisho uliompatia ushindi , Robertson alisema namna familia yake iliyotoka Australia kuwahi fainali hiyo, ilifanya pambano hili kuwa maalum zaidi kwake.

Roberson kwa ushindi huo amejizolea kitita cha paundi za Kiingereza 250,000.