Manchester City yaikanusha Spurs

Manchester City imekanusha vikali madai ya meneja wa Tottenham Harry Redknapp kwamba wanailazimisha Spurs kutoendelea na jitahada zake za kumsajili Craig Bellamy.

Image caption Harry Redknapp aingia matatani na City

Redknapp amedai City ilitishia kulipiza kisasi kwa kumchukua kiungo wao Wilson Palacios wakati ule akiichezea Wigan iwapo Spurs ingekamilisha usajili wa Bellamy aliyekuwa akiichezea West Ham mwezi wa Januari mwaka 2009.

Kwa mujibu wa Redknapp:"City ilisema iwapo hamtoacha jitahada za kumsajili Bellamy, sisi tutamchukua Palacios."

City imewaagiza mawakili wake kuchunguza madai hayo ya Redknapp.

Kwa mujibu wa mwandishi wa BBC Gordon Farquhar, Manchester City imekanusha madai hayo vikali.

"City imesema Wigan iliwafuata kwa ajili ya Palacios, wakati Spurs walikuwa na mawazo ya kumsaini.

Bodi ya Ligi Kuu ya Soka ya England imesema itachunguza madai hayo.

Bellamy alijiunga na Manchester City akitokea West Ham kwa mkataba unaoaminika uligharimu paundi za Kiingereza milioni 14 tarehe 19 mwezi wa Januari 2009, ikiwa ni siku mbili kabla Palacios hajakamilisha mkataba wa paundi milioni 12 kujiunga na Tottenham.

Image caption Mark Hughes na Craig Bellamy

Wapo wanaoamini iwapo Manchester City watafuzu kucheza Ligi ya Mabingwa wa Ulaya msimu ujao, wamiliki wa klabu itawawia rahisi kuvutia wachezaji bora duniani.

Palacios alisainiwa na Wigan kutoka Deportivo Olimpia mwezi Januari 2008 na kocha wa wakati ule wa Manchester City Mark Hughes akamsajili kiungo mlinzi, Nigel de Jong kutoka Hamburg, siku ile ile Tottenham ilipomsajili Palacios .

De Jong ni mmoja kati ya wachezaji walionunuliwa kwa fedha nyingi na City tangu Shirika la Biashara la Abu Dhabi likiungwa mkono na Sheikh Mansour Bin Zayed Al Nahyan, kuafiki kumiliki klabu hiyo tarehe 1 Septemba 2008.

Klabu hiyo ilivunja rekodi ya matumizi ya fedha za usajili kwa Uingereza ilipomchukua Robinho kwa paundi milioni 32.5 akitokea Real Madrid baadae siku hiyo hiyo.

Washambuliaji Carlos Tevez, Emmanuel Adebayor na Roque Santa Cruz walinunuliwa na City msimu uliopita kwa jumla ya paundi milioni 68.