Gareth Barry aumia

Kiungo wa Manchester City na England Gareth Barry anasubiri uamuzi wa daktari bingwa juu ya kuumia kwake kiwiko cha mguu hali inayomuweka njia panda kama ataweza kushiriki mashindano ya Kombe la Dunia.

Image caption Gareth Barry alipoumia

Barry siku ya Alhamisi jioni alikutana na daktari bingwa na baadae atafahamu ukubwa wa tatizo lake.

Kiungo huyo aliumia baada ya kumuagukia mchezaji mwenzake katika kipindi cha pili Manchester City walipofungwa bao 1-0 na Tottenham kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya England siku ya Jumatano.

Meneja wa England Fabio Capello siku ya Jumanne atatangaza majina ya wachezaji 30 wa awali watakaounda kikosi cha England kwa ajili ya Kombe la Dunia.

Capello baadae atapunguza wachezaji na kubakiwa na 23 baada ya mchezo wa kirafiki dhidi ya Mexico na Japan, huku England ikijiandaa kuanza hekaheka za Afrika Kusini watakapopambana na Marekani tarehe 12 mwezi wa Juni.

Barry, ambaye amekwishacheza michezo 36 ya kimataifa, amekuwa mchezaji wa kutumainiwa miongoni mwa wachezaji wa Capello na amekwishaichezea England michezo minane ambayo timu hiyo ilifanikiwa kufuzu kwa Kombe la Dunia.

Tayari kiungo huyo hatoweza kucheza mchezo wa kumalizia msimu huu wa Ligi Kuu ya England dhidi ya West Ham siku ya Jumapili.

Barry ameanza kucheza mechi 43 kwa Manchester City msimu huu, amefunga mabao matatu wakati City ikifanikiwa kufuzu kucheza Ligi ya Europa.

Alijiunga na City mwezi Juni mwaka 2009 akitokea Aston Villa kwa kitita cha paundi milioni 12, akielezea kushindwa kwa Villa kufuzu kucheza Ligi ya Mabingwa wa Ulaya ndio sababu ya kuhama.