Tyson Gay ampania Usain Bolt

Tyson Gay anajiandaa kumshinda hasimu wake Usain Bolt na kumpokonya rekodi yake ya ya dunia ya mita 100 msimu huu wa majira ya joto.

Image caption Tyson Gay aikodolea macho rekodi ya Bolt

Usain Bolt kutoka Jamaica mwaka jana alivunja rekodi ya mita 100 ya sekunde 9.58 katika mashindano ya Ubingwa wa Dunia mjini Berlin.

Gay, aliyeshika nafasi ya pili kwa kutimka kwa m uda wa sekunde 9.71 amesema: "Ninahisi naweza kumshinda. Sijawahi kuona mtu asiyeweza kushindwa.

Ameliambia gazeti la Marekani liitwalo Spikes "Iwapo kuna watu waliowahi kunishinda, kila mara nami nafanya jitahada kuwashinda. "Ndio maana nahisi naweza kumshinda Bolt.

Ameongeza: "Sitarajii hilo kutokea mwaka huu au mwakani lakini ninachotaka siku moja kuvunja rekodi ya dunia.

"Ilikuwa kidogo tu niifikie rekodi ya dunia. Watu wengi wanafikiri haiwezekani lakini ninajitahidi kuivunja.

"Niliridhishwa sana na kiwango changu mwaka 2009. Jinsi nilivyokimbia mbio za mita 100 mjini Berlin imenipa matumaini makubwa na nguvu mpya. Natumai ninayo mengi ya kufanya.

Ushindani

Gay, mwenye umri wa miaka 27, pia amesisitiza Bolt ni binadamu kama binadamu wengine na anaweza kushindwa tofauti na wanavyofikiria watu wengi.

"Hakuna mtu aliye mtimilifu, kila mtu ana upungufu wake," ameongeza. "Ninachoona ni kwamba anakimbia kwa kasi sana ndio sababu kubwa ya kutoweza kumshinda.

"Makocha wengi hawasomi upungufu alionao kwa sababu anakimbia kwa kasi kubwa, lakini nadhani baadhi ya wataalam mahiri wa mbio fupi wanaweza kubaini upungufu alionao."

Gay atakimbia mwezi wa Julai katika mashindano ya Aviva British Grand Prix katika uwanja wa Kimataifa wa Gateshead.