Fifa yaipiga jeki Afrika Kusini

Kiongozi wa Fifa anayesimamia shughuli za Kombe la Dunia za mwaka 2010 amekiri fedha zaidi ya dola milioni 100 zinahitajika kutolewa kwa mradi huo ili kuhakikisha Afrika Kusini haikwami kuandaa mashindano hayo.

Katibu Mkuu wa Fifa Jerome Valcke ameliambia dawati la michezo la BBC kwamba katika mkutano wa kamati kuu uliofanyika mwezi wa Machi shirikisho hilo liliidhinisha nyongeza ya asilimia 25.

Amesema fedha hizo za nyongeza ni kwa ajili ya kuwasaidia Waafrika Kusini kukamilisha kambi za mazoezi kwa timu zitakazoshiriki.

Bajeti ya Afrika Kusini ya kuandaa mashindano hayo sasa imepanda kutoka paundi milioni 282 hadi paundi milioni 349.

Lakini Valcke amesisitiza pato la Fifa la paundi bilioni 2.1 linalotarajiwa kupatikana katika mashindano hayo, zaidi litatumika kuziba pengo la ongezeko la bajeti, ikijumuisha mgao wa Afrika Kusini kutoka paundi milioni 733 hadi paundi milioni 800.

"Viwanja ni maridadi, hali ya msisimko inazidi kupanda na watu niliokutana nao siku chache zilizopita wanasubiri kwa hamu kuwakaribisha wageni kwa moyo mkunjufu," amesema Valke Maafisa wa England wameonesha wasiwasi wao kuhusu sehemu watakayopiga kambi, hasa hali ya uwanja wa kufanyia mazoezi, walipotembelea kampasi ya michezo ya Royal Bafokeng mwezi wa Desemba.

Lakini meneja wa England Fabio Capello inafahamika ameridhika kwamba kampasi hiyo ipo tayari kupokea timu yake mwezi ujao.