Zola atimuliwa West Ham

West Ham imemtimua meneja wake Gianfranco Zola baada ya kuifundisha kwa kipindi cha chini ya miaka miwili.

Image caption Zola atimuliwa West Ham

Zola mchezaji wa zamani wa Chelsea ambaye hakuwa na ujuzi wa umeneja wa soka siku za nyuma kwa kiwango cha vilabu, alichukua nafasi ya kuifundisha West Ham kutoka kwa Alan Curbishley mwezi wa Septemba mwaka 2008.

Aliingia mkata wa miaka minne kuifundisha klabu hiyo mwishoni mwa muhula wake wa kwanza ambapo West Ham ilimaliza nafasi ya tisa ya msimamo wa Ligi Kuu ya England.

Lakini msimu huu timu hiyo iliyumba na imemaliza katika nafasi ya 17, ikiwa ni pointi tano tu nyuma ya shimo la kuteremka daraja.

Taarifa iliyotolewa na West Ham imesema: "West Ham United inathibitisha kukatiza mkataba na Gianfranco Zola.

"Bodi ya Wakurugenzi ingependa kumshukuru kwa mchango wake na inamtakia kila la heri aendako.

"Klabu kwa sasa inaelekeza jitahada zake kumtafuta mtu atakayechukua nafasi yake.

Taarifa ya West Ham imesema baada ya tangazo hilo haitazungumzia tena suala hilo.

Nafasi ya Zola katika klabu hiyo ya mashariki mwa London ilikuwa mashakani baada ya klabu hiyo kuchukuliwa na David Gold na David Sullivan mwezi Januari 2010.

Sullivan, ambaye awali alikuwa mmiliki mwenza wa klabu ya Birmingham City, aliita timu ya Zola ya West Ham kama ni ya "kusikitisha" baada ya kufungwa mabao 3-1 na Wolves.

Na alipoulizwa hatma ya Zola baada ya mechi hiyo, Sullivan alijibu: "Nisingependa kuzungumzia suala hilo, lakini hakuna ajuaye."