Onuoha ahitaji kuchezea Nigeria

Mlinzi wa Manchester City Nedum Onuoha amesisitiza hajakataa kuichezea timu ya taifa ya Nigeria.

Image caption Onuoha na Sylvinho wakimkabili Peter Crouch

Shirikisho la Soka la Nigeria lilieleza kuwa Onuoha alikataa maobi ya kujiunga na kikosi cha Nigeria kitakachocheza Kombe la Dunia nchini Afrika Kusini.

Onuoha amekwishachezea timu ya taifa ya England chini ya miaka 21, lakini anaweza kuichechezea Nigeria kwa vile tu hajawahi kuchezea timu ya wakubwa ya taifa ya England.

Mchezaji huyo bado hajaamua ni nchi gani aichezee inapofika kiwango cha timu ya wakubwa.

"Ninachosema nahitaji kuweka mambo sawa katika klabu yangu ili niwe mchezaji wa kudumu wa kikosi cha kwanza kabla kufikiria masuala ya kimataifa," amesisitiza.

Onuoha alishangazwa pia na namna taarifa hiyo ilivyokuwa imetangazwa.

Ameongeza:"Nilimueleza meneja wa Nigeria si wakati muafaka kwangu, lakini baada ya hapo kukazuka hisia tofauti nchini Nigeria na kabla ya hapo watu wakaanza kusema naipa kisogo England."

"Lakini najaribu kufika mahala ambapo nitaweza kucheza michezo mingi na kucheza vizuri ili niweze kuwa na chaguo la kuchezea ama Nigeria au England. Kwa hiyo ni bora nikajikita katika hali hiyo kwanza kabla sijafanya uamuzi."

Onuoha amekanusha ripoti zilizosema amekataa kuichezea Nigeria kwa sababu anasubiri kuteuliwa na Fabio Capello katika timu ya taifa ya England.

"Kwa kwweli nilishtuka kwa sababu hakuna ukweli katika hilo. Hiyo kamwe haikuwa sababu yangu ya kufanya uamuzi."