Ballack kutocheza Kombe la Dunia

Nahodha wa Ujerumani Michael Ballack hatacheza Kombe la Dunia kwa sababu ya kuumia kiwiko cha mguu wa kulia wakati wa mchezo wa fainali ya kombe la FA siku ya Jumamosi.

Ballack mwenye umri wa miaka 33 anayechezea pia Chelsea, tayari amekwishaiwakilisha Ujerumani katika michezo 98 na pia ameichezea timu yake hiyo ya taifa katika fainali mbili za Kombe la Dunia.

Kipimo alichofanyiwa kimeonesha amechanika kidogo kano ya mguu, lakini anatazamiwa kuwa nje ya dimba kwa takriban wiki nane kabla hajaanza mazoezi na Ujerumani mchezo wake wa kwanza katika Kombe la Dunia ni tarehe 13 mwezi wa Juni.

Alijeruhiwa baada ya kukabiliwa na mchezaji wa Portsmouth Kevin-Prince Boateng.

Image caption Ballack alipoumizwa na Boateng

Kevin-Prince Boateng huenda akawemo katika kikosi cha timu ya taifa ya Ghana ambacho kimepangwa kundi moja la D na Ujerumani nchini Afrika Kusini.

Boateng mchezaji wa zamani wa Tottenham alizaliwa Ujerumani na ameiwakilisha nchi hiyo katika timu ya vijana, lakini amechagua kuichezea Ghana, nchi alikozaliwa baba yake.

Baada ya Fifa kuondoa kikwazo cha umri kwa wachezaji wanaotaka kuhamishia uraia wao nchi nyingine, Boateng mwenye umri wa miaka 23 ameruhusiwa kuichezea Ghana katika fainali za Kombe la Dunia na ameteuliwa katika kikosi cha awali cha wachezaji 30.

Maumivu ya Ballack

Baada ya kukabiliwa na Boateng katika dakika ya 35 uwanja wa Wembley, Ballack alitolewa nje akiwa anachechemea.

Kipimo cha awali cha X-ray kilichofanywa uwanjani, kilionesha hakuna mfupa uliovunjika, lakini kipimo zaidi kilichofanyika nchini Ujerumani siku ya Jumatatu kimeonesha ukubwa wa tatizo.

Shirikisho la soka la Ujerumani limesema Ballack itambidi avae kiatu maalum kwa wiki mbili.

Taarifa ya Chelsea imethibitisha: "Daktari wa timu ya taifa ya Ujerumani Hans-Wilhelm Muller-Wohlfahrt, amekadiria Balack anaweza kurejea uwanjani mapema ni baada ya wiki nane."

Ujerumani itaanza hekaheka za Kombe la Dunia dhidi ya Australia tarehe 13 mwezi wa Juni kabla ya kukabiliana na Serbia tarehe 18 Juni na Ghana tarehe 23 mwezi wa Juni.