Argentina na Korea Kusini zashinda

Image caption Gabriel Heinze akishangilia goli pekee la Argentina dhidi ya Nigeria.

Diego Maradona ameukumbusha ulimwengu kwamba ana kikosi chenye uwezo wa kunyakua Kombe la Dunia, baada ya timu yake kuifunga Nigeria bao 1-0.

Mechi hiyo katika uwanja wa Ellis Park ilikuwa ya pili kwenye kundi B, na ilitanguliwa na mchuano kati ya Korea Kusini na Ugiriki, ambapo Korea Kusini walishinda 2-0.

Bao la Argentina dhidi ya Nigeria lilifungwa kwa kichwa katika dakika ya 6 na mlinzi Gabriel Heinze kufuatia mpira wa kona.

Mchezaji bora duniani, Lionel Messi, alikuwa amepenya ngome ya ulinzi ya Nigeria, akatandika mkwaju ambao mlinda mlango Vincent Enyeama aliutema nje, hivyo Argentina wakapata kona iliyozaa bao hilo.

Ngome ngumu

Katika kipindi cha pili timu zote zilizidisha mashambulizi bila mafanikio.

Peter Odimwingie aliyeingia katika kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Chinedu Obasi aliipenya ngome ya Nigeria na kutoa kombora kali ambalo kipa wa Argentina, Sergio Romero, alilazimika kupangua.

Argentina pia walifanya mashambulizi ya mara kwa mara katika kipindi cha pili, lakini mashuti ya Carlos Tevez na Lionel Messi yalikabiliwa na ngome ya Nigeria.

Awali katika kundi B, Korea Kusini iliifunga Ugiriki mabao 2-0 katika uwanja wa Port Elizabeth.

Kwa sasa katika kundi hilo la B Korea Kusini inaongoza ikifuatwa na Argentina, Nigeria na Ugiriki.