Kombe la Dunia: Ratiba ya duru ya pili

Image caption Marekani watacheza na Ghana mwakilishi pekee wa Afrika aliyesalia katika michuano hiyo.

Michuano ya raundi ya pili ya Kombe la Dunia nchini Afrika Kusini inaanza Jumamosi, huku timu 16 zilizofuzu hatua hiyo zikiwania nafasi nane za robo fainali.

Siku ya Jumamosi katika uwanja wa Nelson Mandela Bay mjini Port Elizabeth, Uruguay itacheza na Korea Kusini, mechi itakayoanza saa 14.00 GMT ambayo ni sawa na saa kumi na moja jioni kwa saa za Afrika Mashariki.

Baadaye siku hiyo saa 18.30 GMT au tatu unusu usiku Afrika mashariki, katika uwanja wa The Royal Bafokeng mjini Rustenburg, Ghana na Marekani zitachuana kutafuta nafasi ya robo fainali.

Siku ya Jumapili tarehe 27 kuna michuano miwili ya raundi ya pili.

Mechi ya mapema katika uwanja wa Free State mjini Bloemfontein, itakutanisha mahasimu wa jadi, Ujerumani na England. Mechi itaanza saa 1400 GMT, sawa na saa kumi na moja jioni, Afrika Mashariki.

Siku hiyo hiyo jioni mjini Johannesburg, mabingwa mara mbili Argentina watakutana na Mexico. Mechi hiyo itaanza saa 1830 GMT au saa tatu unusu kwa saa za Afrika mashariki.

Jumatatu tarehe 28 mjini Durban Uholanzi ambayo ilishinda mechi zake zote katika kundi E itachuana na Slovakia, iliyowaondoa mabingwa watetezi Italia. Hiyo itakuwa mechi ya mapema.