Serena atwaa taji la tennis Wimbledon

Image caption Serena Williams ameshinda taji lake la nne la Wimbledon.

Serena Williams ameshinda taji lake la nne la ubingwa wa Wimbledon katika mchezo wa tennis kwa kumshinda Vera Zvonareva wa Urusi kwa seti mbili kwa mfuto katika fainali ya wanawake. Hii inakua ni mara ya 13 kwa Serena kunyakua ubingwa wa mashindano makuu ya kimataifa ya Grand Slam.

Serena ambaye ndiye mchezaji nambari moja dunia alitetea taji lake dhidi ya mrusi huyo 6-3, 6-2 katika muda wa dakika 67 na kuongeza udhibiti wa familia ya Williams katika Wimbledon. Serena amemaliza mashindano ya mwaka huu bila ya kupoteza hata seti moja na kuongezea mataji aliyokwishajinyakulia ya Wimbledon katika miaka ya 2002, 2003 na 2009.

Hii ni mara ya kwanza kumshinda mtu ambaye si dada yake Venus katika fainali ya Wimbledon. Dada hawa wawili kwa jumla wameshinda mara tisa ubingwa wa Wimbledon katika miaka 11 iliyopita.